Na Aron Msigwa – MAELEZO
WANAFUNZI wanawake wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE) wamezindua mchakato wa kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Kike wenye lengo la kumkomboa na kumwezesha mwanafunzi wa kike kujitambua, kielimu, kisiasa na kiutamaduni.
Akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Kike wa chuo hicho wakati kwenye uzinduzi wa mfuko huo leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk. Mery Mwangisa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amesema kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni ishara ya umoja na mshikamano wa wanafunzi wa kike chuoni hapo.
Alisema kuanzishwa kwa mfuko huo kunatokana na kuongezeka kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake pia kukosekana kwa mifuko ya aina hiyo katika taasisi nyingi za elimu ya juu hapa nchini.
Alisema kuwa malengo ya mfuko huo ni kumwezesha mwanafunzi wa kike wa CBE kujitambua kielimu, kisiasa na kiutamaduni na kuongeza kuwa yamekuja wakati muafaka kufuatia mabadiliko yaliyopo sasa ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni. Alifafanua kuwa mfuko huo ulioanzishwa ni fursa pekee ya kuwawezesha wanafunzi wa kike kunufaika kwa kupata elimu bora bila vikwazo.
“Napenda kutumia fursa hii kuushukuru uongozi wa chuo hiki kwa kuonyesha njia ya kuwajali wanawake na pia katika kuweka taratibu nzuri za kulinda maadili, katika maisha yangu sijawahi kusikia chuo kikuu chochote kimezindua jukwaa la wanawake lenye malengo mazuri kama yenu,” Alisema Dk. Mwangisa.
Aidha alisema kuwa kwa muda mrefu wanawake kote nchini wamekuwa na juhudi mbalimbali za kujikomboa kiuchumi pamoja na kulitumikia taifa kwa kushika nyadhifa mbalimbali serikalini kwa ufanisi mkubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii pindi wanapokabidhiwa madaraka.
“Ninapowaangalia ninyi nafarijika maana naona viongozi wakuu wa serikali, naona marais na pia wakurugenzi wa biashara,”
Akizungumza kuhusu kuanzishwa kwa mfuko huo na mafanikio yake Dk. Mwangisa alisema kuwa atatoa ushirikiano kwa wanafunzi hao ili kuhakikisha kuwa mfuko huo unajengewa uwezo wa kusimama na kuwanufaisha wanawake wanaokumbwa na changamoto zinazokwamisha maendeleo yao ikiwemo ukosefu wa fedha.
Alisema kukamilika kwa taratibu za jumuiya hiyo ikiwemo maandalizi ya katiba ya jukwaa hilo kutaliwezesha jukwaa hilo kupanga, kuandaa na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kujiendesha ili kuwawezesha wanafunzi hao kutatua changamoto zinazowakabili kwa kulinda heshima yao katika jamii.
Kwa upande wake mjumbe wa Bodi ya Taaluma ya Chuo hicho Dk. Ellen Oturu Okoedion amesema kuwa wanafunzi wa kike wa chuo hicho wanahitaji msaada kupitia mfuko huo utakaowawezesha kupambana na wimbi la wanafunzi wa kike kushindwa kumaliza masomo yao kwa kushindwa kumudu gharama za masomo.
Hata hivyo amewataka wanafunzi wa kike wa chuo hicho kutumia ipasavyo taaluma wanayoipata kusaidia mfuko huo kupata fedha ili uwe endelevu kwa maendeleo ya wanawake na chuo hicho.
“Ninyi mnasoma elimu ya biashara na ndio watalaam wenyewe sitarajii mfuko wenu ukose uwezo, naamini mtatumia taaluma yenu mnayoipata hapa chuoni kutafuta fedha kwa kuwa mnao uwezo huo,” Alisisitiza Dk. Ellen.
Naye Waziri wa Wanawake wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Bi. Mwajuma Sangali ameeleza kuwa wanawake kote nchini wana jukumu la kuandaa kizazi cha watu wenye upendo, uzalendo, kupenda kazi na maendeleo. Alisema kuanzishwa kwa chombo hicho kunalenga kuboresha maisha ya wanawake hasa katika masuala ya elimu, jamii, uchumi na siasa.