Wanafunzi Rombo Wagomea Chakula cha ‘Wadudu’ Shuleni

Baadhi ya wanafunzi Wilayani Rombo Wakiwa kwenye foleni ya kuchukua chakula cha mchana shuleni. Wanafunzi hawa si waliogomea chakula.

Yohane Gervas, Rombo

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari Kwaikuru iliyopo katika wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wamegoma kula chakula cha mchana shuleni hapo kwa kile walichodai kuwa chakula hicho kina wadudu.

Tukio hilo lilitokea Julai 19, mwaka huu shuleni hapo jambo ambalo lilivuta hisia za watu wengi. Wanafunzi hao wakizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti walisema kuwa mara kadhaa sasa wamekua wakikuta wadudu kwenye chakula na kuvumilia, lakini jana chakula hicho kilionekana kimezidi wadudu hali iliyowafanya wanafunzi hao kushindwa kula na kugoma.

Hata hivyo baadaye baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha pili waliridhia kula chakula hicho, huku wa kidato cha tatu na nne wakigomea kabisa chakula hicho.

Aidha wanafunzi hao wameiomba serikali kupitia idara ya Afya kufanya ukaguzi wa haraka wa chakula shuleni hapo ili kuwanusuru afya zao kwani hali ni mbaya. Wamefafanua kuwa endapo hali hiyo ikiendelea huenda afya zao zikawa hatarini.

Baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao waliozungumza na mtandao huu kwa masharti ya kutotaja majina walisema kuwa wanashangazwa wao kulipia kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya chakula lakini wanafunzi hawapewi chakula kizuri na matokeo yake kupikiwa kikiwa na wadudu.

“Tunalipia 80,000 kwa ajili ya chakula lakini hatuoni cha maana wanalishwa wadudu tunaomba serikali iingilie kati,” alisema mzazi mmoja aliyekataa kutaja jina lake. Juhudi za kumpata mkuu wa shule hiyo kuzungumzia mgomo huo hazikuzaa matunda.