Yohane Gervas, Rombo
ZAIDI ya wanafunzi 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2013 ambao wangetakiwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu (2014) hadi sasa bado hawajaripoti katika shule walizopangiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Elinasi Pallengyo amesema kuwa kati ya wanafunzi 558 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza hadi sasa bado hawajaripoti shuleni kati yao ni wasichana 265 na wavulana 293. Alisema kuwa idadi hiyo ni kubwa na hivyo serikali katika Wilaya ya Rombo, inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wazazi waliogoma kuwapeleka wanafunzi shuleni wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vinavyohusika.
Aidha Pallengyo alisema kuwa kutokana na hali ya utoro wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kuzidi kuongezeka halmashauri ya Wilaya ya Rombo imedhamiria kutunga sheria ndogo ya kusimamia elimu ya sekondari. Pia katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amewataka wananchi wilayani humo kutumia vizuri mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali wilayani Rombo kupanda mazao ya muda mfupi na mazo mengine yanayostahimili ukame.