Na Mwandishi Wetu, Moshi
WANAFUNZI 48 wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lyakirimu iliyoko Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro wamenusurika kifo baada ya bweni walilokuwa wakiishi kuteketea kwa moto.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea Mei Mosi majira ya saa Mbili na nusu usiku wakati wanafunzi hao wakiwa kwenye chumba cha kusomea.
Kamanda alisema chanzo cha moto huo ni itilafu ya umeme ambapo vitu vyote vilivyokuwa katika bweni hilo ikiwemo vitanda 48,magodoro 48 na vifaa vya wanafunzi viliteketea.
Aidha kamanda alisema pamoja na mali hizo kuteketea wanafunzi 14 walipata mstuko ambapo walikimbizwa katika zahanati ya Marangu ili kupatiwa matibabu. Alisema Kutokana na moto huo hakuna madhara makubwa yaliyotokea ambapo moto huo ulifanikiwa kuzimwa na wananchi na jumuiya ya shule.
Kamanda alisema uchunguzi unaendelea ili kuweza kujua kama kulikuwa na hujma katika tukio hilo au la na kwamba thamani ya vitu vyote vilivyoungua bado haijajulikana. Kwa mujibu wa habari zilizopatikana ni kwamba Bweni hilo lililoteketea lilikuwa na itilafu ya umeme kwa muda wa siku mbili ambapo taa zilikuwa haziwaki hadi ilipotokea ajali hiyo na kuteketeza mali zote zilizokuwemo.