Wanafamilia waandamana kuipinga Serikali ya Kijiji

Machimbo ya mchanga


Na Mwandishi Wetu, Arumeru

WANAFAMILIA kutoka katika familia mbili tofauti kutoka Kata ya Engorora wilayani hapa jana waliandamana hadi ofisi za kijiji chao wakidai fedha za malipo yanayotokana na uchimbaji wa moramu, kwenye eneo ambalo wanadai ni mali yao.

Wakizungumza jana na waandishi wa habari eneo hilo, mmoja wa wanafamilia, Wilbert Levosi alidai wao ndiyo wamiliki halali wa mlima huo unaochimbwa moramu ambao huiingizia Serikali ya Kijiji hicho sh. 700 kwa kila tani inayouzwa.

Alidai kuwa serikali ya kijiji hicho mwaka 1985 iliyokuwa ikiongozwa na mwenyekiti wake Elisha Sheshe aliyefariki 1989 iliidhinisha familia hizo mbili kupewa sehemu ya malipo inayotokana na ushuru wa moramu hiyo ambapo walikubalina kupewa sh. 200 kwa tani moja.

Alisema kuwa hadi hivi sasa hawapatiwi kiasi chochote cha fedha ambapo serikali ya kijiji hicho pia imetoa kibali kwa kampuni za simu za mikononi kuweka minara yao juu ya mlima huo ambao hutozwa kiasi cha sh. milioni 3 kwa mwezi bila wao kupewa kiasi chochote.

Alidai walilazimika kwenda katika ofisi hizo ambapo kamati ilikaa na kuamuru wapewe hekari 200 ili kupisha eneo hilo na kuonyesha gazeti hili nakala ya barua inayoonyesha kutolewa Machi 3 mwaka 2011 ili eneo hilo liendelee kuwa chanzo cha mapato kwa serikali na agizo hilo kupitsihwa na mkutano mkuu wa kijiji.

Kwa upande wajke Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Joseph Laizer, alisema kuwa yeye ni kiongozi tngu mwaka 2004 na alipokabidhiwa toka uongozi uliopita hakuambiwa kama hiyo mali ya hizo familia mbili kama wanavyodai.

Kiongozi huyo alisema ni vema wananachi wakafahamu badala ya kuleta vurugu za kuzuia watu kuendelea na shughuli za uchimbaji na badala yake kuwataka wafuate kanuni na sheria za nchi.

Akizungumzaia madai ya kila familia kupewa hekari 100 alikanusha vikali madai hayo na kusema kuwa madai hayo hayana ukweli wowote kwani kijiji hicho hakina hata hekari hizo za kuwafidia wananchi hao na kudai kuwa wanatoza ushuru wa sh. 200 na siyo 700.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Khalifa Hidda, akizungumzia tukio hilo alidai kushangazwa na hatua waliyofikia wananchi hao na kuongeza kuwa mlima huo ni mali ya Serikali na umeanza kuchimbwa moramu hiyo mwaka 1920.

Hidda alifafanua kuwa wamejitokeza watu wachache wanaodai mlima huo ni mali yao jambo ambalo siyo kweli, ambapo alisema kuwa alipigiwa simu na Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mecy Silla akimweleza tukio hilo la wananchi kuvamia ofisi za kijiji zilizopo karibu na machimbo hayo na kuzuia uchimbwaji kuendelea.