Wamuhakikishia Dk. Shein Kupambana na Dawa za Kulevya na Ukimwi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais katika utekelezaji wa kazi za Ofisi hiyo katika Ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Zanzibar.[Picha na RamadhanOthman, Ikulu]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

OFISI ya Makamu wa Kwanza wa Rais imemuahidi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kuwa itashirikiana naye katika kusimamia majukumu yake kwa uadilifu na bidii ili jamii isiendelee na kuathiriwa utumiaji wa dawa za kulevya, UKIMWI, uharibifu wa Mazingira na kuwajumuisha watu wenye ulemavu.

Maelezo hayo yametolewa na uongozi wa Wizara hiyo, wakati wa mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa Malengo Makuu ya Wizara hiyo kwa kipindi cha Aprili- Juni 2011-2012 na Julai- Septemba 2012-2013.

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Kwanza Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahaya Mzee walishiriki kikamilifu.

Akisoma taarifa ya utangulizi ya utekelezaji wa Malengo makuu hayo ya Wizara, Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Fatma Fereji alitoa shukurani kwa Rais pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye ndiye msimamizi mkuu wa Ofisi hiyo pamoja na na Makamu wa Pili wa Rais kwa miongozo wanayowapa katika kutekeleza majukumu yao.

Waziri Fereji, alisema kuwa juhudi za Dk. Shein ndizo zinazoupelekea uongozi wa Ofisi hiyo kuwa na msukumo na hamasa katika kufanikisha malengo waliyojiwekea.

Ofisi hiyo ilimuahidi Dk. Shein kuwa itaendelea kumuunga mkono katika kufanikisha juhudi hizo ili Zanzibar iwepo bila ya dawa za kulevya, na kuwa mfano katika uhifadhi wa mazingira, udhibiti wa maambukizi mapya ya UKIMWI na kuwa na jamii jumuishi.

Akieleza mafanikio yaliopatikana katika Wizara hiyo, Mhe. Fereji alisema kuwa ni pamoja na kukamilika kwa tovuti ya Ofisi ya Makamu wa Kwaza wa Rais, kukamilika kwa Kanuni ya Mifuko ya plastiki na kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali Namba 113 la mwaka 2011.

Mafanikio mengine ni pamoja na kukamilika kwa muongozo wa kuanzisha nyumba za makaazi kwa wanaotaka kuacha kutumia dawa za kulevya yaani sober houses, muongozo huu ambao utasaidia katika kuleta ufanisi na uwiano wa utoaji wa huduma za makaazi kwa vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya.

Kuundwa kwa kamati za kitaalamu na usimamizi ya mabadiliko ya tabia nchi, pia, ni miongoni mwa mafanikio ambapo kamati hizo pamoja na mambo mengine zitakuwa zinaratibu usimamizi wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaandaliwa.

Mafanikio mengine ni pamoja na kumalizika kwa usajili wa watu wenye ulemavu katika mikoa yote miwili ya Pemba na Mkoa wa Kaskazini Unguja, taarifa ambazo zitaweza kusaidia taasisi mbali mbali za Serikali, zisizokuwa za serikali na mashirika binafsi katika kupanga mipango ya kimaendeleo.

Kuanzisha maafisa waratibu wa masuala ya Watu Wenye Ulemavu pamoja na kukamilika na kuzinduliwa kwa Mkakati wa pili wa Taifa wa UKIMWI, mkakati huu ndio unaotoa muongozo wa utekelezaji wa mapambano dhidi ya ya UKIMWI kwa kipindi cha miaka mitano.

Mbali ya mafanikio hayo, Ofisi hiyo pia ilieleza changamoto zake inazozikabili huku ikieleza jinsi juhudi inazozichukua katika kupambana nazo ikiwa ni pamoja na namna ya kuwa na matumizi endelevu ya kuvuna maliasili zisizorejesheka pamoja na uingizaji wa bidhaa chakavu uliokithiri.

Kutofuata utaratibu wa uchunguzi wa athari za kimazingira kabla ya kuanza miradi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuathiri shughuli za wananchi kwenye kilimo, huduma ya maji ya kunywa na uvuvi.

Aidha, Wizara hiyo ulieleza changamoto iliyopo katika uingizaji na utumiaji wa dawa za kulevya pamoja na udhalilishaji wa watu wenye ulemavu, unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI pamoja na makundi maalumu ambao unajitotokeza katika kutumia huduma za kinga na tiba ipasavyo.

Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa kwa Ofisi hiyo kutokana na mafanikio iliyoyapata katika utekelezaji wa Mpango kazi. Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuzifanyia kazi changamoto zilizopo kwa kuwashirikika miongoni mwa wadau husika.