Wamiliki wa Magari ya Mizigo Wasema Hawajagoma, Ila Wanaogopa….!

IMG_0164

Baadhi ya wamiliki wa magari ya mizigo wanaodaiwa kugoma wakizungumza na waandishi wa habari.

IMG_0204

 

Mwanasheria wa wamiliki wa magari ya mizigo (kulia) akifafanua jambo wakati wateja wake walipozungumza na waandishi wa habari.

IMG_0186

IMG_0181

 

Waandishi wa habari kutoka vyombo anuai vya habari wakifuatilia mkutano huo na wamiliki wa malori jijini Dar es Salaam.

 

WAMILIKI wa magari ya mazigo wanaodaiwa kuendesha mgomo ikiwa leo ni siku ya nne tangu kuanza kwa mgomo huo wamejitokeza kwa waandishi wa habari na kudai kuwa wao hawajagoma bali wamepumzisha magari yao (malori) ili kuepusha kitendo cha kuendelea kuharibu barabara za lami. Wamiliki hao wametoa kauli hiyo walipokutana na waandishi wa habari katika ukumbi wa habari maelezo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mmoja wa wamiliki hao, Azim Dewji alisema wataendelea kupumzisha magari yao hadi pale Serikali itakapokubali kuondoa asilimia tano ya uzito inayolalamikiwa na wadau hao tangu iamuriwe kuanza kutumika katika magari ya mizigo. Alisema kwa sasa mzigo wowote ambao utabebwa na magari yao kutoka bandarini utaonekana umezidi utakapo pimwa kwenye mzani kutokana na punguzo la asilimia tano hivyo ili kuepusha mgogoro huo na Serikali wamelazimika kupaki magari yao wakisubiri ombi lao la kutaka mabadiliko hayo yasitishwe na utaratibu kuandaliwa upya kwa kushirikisha wadau wote.

Alisema madai ya kwamba wao si wazalendo na wanafurahia kuharibika kwa barabara za lami kutokana na kitendo cha kuzidisha mizigo kinachoelezwa na baadhi ya viongozi si ya kweli kwani wao ni wanufaika namba moja wa barabara nzuri kutokana na biashara zao hivyo hawawezi kuwa sehemu ya wanaohujumu uharibifu wa barabara hizo. “Barabara zinapokuwa nzuri ni manufaa kwa kila mwananchi, lakini sisi ni wanufaika namba moja wa barabara hizo kutokana na kuzitegemea zaidi, hivyo hatuwezi kuzihujumu hata siku moja,” alisema Dewji.

Aidha mdau mwingine wa magari ya mizigo Deus Mosha alisema yapo maombi mbalimbali ambayo siku zote wanayatoa kwa Serikali ili kuondoa mgogoro wa uzito wa mizigo na magari lakini hayazingatiwi. Alisema wamewahi kushauri uwepo wa kituo cha mzani bandarini ili magari yote yapime mara baada ya kupakia mizigo na takwimu zihifadhiwe na kutumika kulinganisha utofauti kutoka mzani mmoja na mwingine jambo ambalo lingeweza kupunguza mgongano lakini haijawahi kufanyiwa kazi.

Aliongeza kuwa wao ni wastarabu na ndiyo maana wamekutana na viongozi wa Serikali na kuwasilisha hoja zao na maombi ya kusitishwa kwa mabadiliko hayo ya asilimia tano kwa sasa ili mazungumzo na maandalizi yafanywe kwa kushirikisha wadau wote kabla ya kukazaniwa kwa mabadiliko hayo. “Tunaamini kuwa Serikali yetu ni sikivu hivyo itazingatia maombi yetu ili tuendelee na biashara…hatufurahi tunavyoona shughuli mbalimbali zinaanza kudorora kutokana na huduma zetu kusimaa, sekta yetu inagusa sehemu kubwa ya uchumi wa nchi hivyo hatutaki hali hii ya mvutano iendelee,” alisema Mosha.

Hata hivyo wamesema wanashangaa ukimya uliopo tangu kuanza kwa mgogoro huo ilhali kwa sasa mabasi ambayo nayo awali yaligoma kutokana na mabadiliko hayo yameruhusiwa kufanya kazi na kutopima uzito wakati mazungumzo yakifanywa kati ya wadau wa pande zote. “Tusimame kwenye sheria wanaoumia kwa sasa kutokana na kusimama kwa huduma ya maroli ni wengi hivyo kuna kila sababu ya mgogoro huu kutatuliwa mapema,” alisema Mosha.