Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Mbeya
TAASISI ya Wanawake na Maendelea (WAMA) imetoa msaada wa cherehani ya kudarizi kwa mjane Fatma Almasi ambaye ni mkazi wa Ilomba jijini Mbeya. Makabidhiano ya Cherehani hiyo yalifanyika hivi karibuni Ikulu jijini Mbeya.
Akimkabidhi cherehani hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA alisema kuwa moja ya kazi anazozifanya ni kumuinua mwanamke kiuchumi hivyo basi alitoa cherehani hiyo ili iweze kumsaidia mjane huyo katika maisha yake.
Mama Kikwete alisema kuwa cherehani hiyo ni moja ya vyerehani walivyovipata kutoka nchini China kwani watu wanapoomba kusaidiwa siyo kama vitu wanavyovihitaji vipo bali nao wanatafuta sehemu mbalimbali wakipata wanafikisha kwa wahitaji.
“Nakutakia kila la heri katika kazi zako ila usisahau kuleta mrejesho kama kazi inaendelea au la, isije ikatokea baada ya muda cherehani ikauzwa hiyo siyo maana yake bali ifanye kazi ya kuzalisha ili nawe uweze kujiinua kiuchumi,” alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Fatma Almasi alimshukuru Mama Kikwete kwa msaada aliompatia kwani amekuwa akihitaji kuwa na cherehani ya kudarizi kwa kuwa uwezo wa kudarizi anao lakini hakuwa na kitendea kazi na aliahidi kuongeza cherehani kingine kutokana na nguvu zake mwenyewe. Fatma alisema, “Kinamama tujitahidi kujikwamua kimaisha kwani mwanamke akiwezeshwa anaweza,
tusiwe wategemezi kwa kina baba na mtu asijione kuwa yeye ni mjane au anaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) hawezi kufanya jambo lolote na kuona kuwa ni mwisho wa maisha bali ajitahidi kuwa mjasiriamali kwa kufanya hivyo ataweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha”.
Aliwaomba wanawake kumuunga mkono na kumtia nguvu Mama Kikwete kwani ana moyo wa huruma na upendo wa kuwasaidia kina mama na watoto wa kike. Taasisi ya WAMA imekuwa ikiwainua wanawake kiuchumi, kutoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike ambao hawakupata nafasi ya kusoma, kuimarisha afya ya mama wajawazito na watoto na kuwasaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.
VIONGOZI wa Serikali, Dini na Vyama vya Siasa nchini wametakiwa kuondoa tofauti zao na kutumia majukwaa kuhubiri amani na upendo ili kudumisha mshikamano na utulivu ndani ya jamii.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mchungaji wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Itiri Daniel Siame wakati wa ibada ya mazishi ya Ditective Sagenti Christopher Kyendesya aliyefariki Juni 19 mwaka huu wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa ajali ya Pikipiki.
Mchungaji Siame alisema kuwa Serikali haina dini bali jamii ndiyo inadini mbalimbali zikiwemo za Ukristo, Uislamu na Upagani na kuwaomba viongozi hao pale wanapokutana na wananchi kuhubiri mambo yanayompendeza Mwenyezi Mungu.
“Inawezekana kuwa ndani ya dini zetu kuna watu ambao wanamapokeo ya dini tu na siyo kumtangaza Mwenyezi Mungu hivyo basi sisi kama viongozi wa Serikali, Dini na Vyama vya siasa tunakazi kubwa ya kutangaza mambo ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na amani na siyo mambo ya uchochezi”, alisema Mchungaji Siame.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alimshukuru mchungaji huyo kwa kuwahimiza watu wote wakiwemo viongozi na wananchi kuhusu umuhimu wa amani na upendo katika jamii.
Kandoro alisema kuwa ni jukumu lao viongozi wa Serikali, Dini na wanasiasa kutumia lugha ya kuwajenga watanzania ili waone kuwa amani ni silaha ya maisha yao ya kila siku kwani ikivurugika msingi mkubwa wa maisha unaharibika na hakuna hata mmoja atakayefurahi kuona kuwa amani na upendo vinatoweka.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ni miongoni mwa viongozi mbalimbali waliohudhuria mazishi hayo wakiwemo pia maofisa wa Jeshi la Polisi, wanasiasa na watendaji wa Serikali.