Na Anna Nkinda – Maelezo, Nachingwea
JUMLA ya mikopo yenye thamani ya bilioni 1.9 zimetolewa kwa wanachama wa vikundi vya kukopa na kuweka akiba vilivyopo chini ya mradi wa Mwanamke Mwezeshe unaosimamiwa na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA).
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa kuanzishwa kwa vikundi vya mradi wa Mwanamke Mwezeshe zilizofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Ualimu Nachingwea mkoani Lindi.
Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alisema fedha zilizotolewa katika mkopo huo zimevuka lengo la kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 534 kwa mwaka na katika wilaya ya Nachingwea mikopo yenye thamani ya shilingi 326,442,464/= ilitolewa.
“Kutokana na kilio cha wanawake wengi na wafanyabiashara wadogo wadogo cha ukosefu wa mikopo yenye masharti naafuu mradi huu ulianzishwa na kuwawezesha wanavikundi vya hisa kukopeshana kwa masharti naafuu ikiwemo kiasi kidogo cha ziada ya mkopo ambayo kwa lugha ya kibenki huitwa riba,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alifafanua kuwa mradi wa Mwanamke Mwezeshe ambao ulianza kufanya shughuli za kijamii mwanzoni mwa mwaka jana katika wilaya za Rufiji, Kilwa, Liwale, Lindi vijijini, Nachingwea kwa ufadhili wa Financial Sector Deeping Trust (FSDT) unalenga kuanzisha vikundi 3000 vyenye jumla ya wanavikundi 60,000 kwa kipindi cha miaka mitatu.
Alisema mradi huo pia umetoa ajira kwa wakazi wa maeneo ya mradi wapatao 120 ambao kati ya hao 48 wapo wilaya ya Nachingwea ambao wamepata mafunzo ya ukufunzi wa wanavikundi na sasa wanafanya kazi ya kutoa elimu kwa vikundi katika maeneo yao.
Mama Kikwete alisema, “Vikundi hivi ni msingi mzuri wa kufanikisha jitihada za kupunguza umaskini wa kipato kwa wanawake, ni mfumo unaowezesha kuwafikia watu wengi zaidi kwa muda mfupi na huwavutia watoa huduma za jamii kwani mtandao wa vikundi hivi unarahisisha kuwafikia wananchi”.
Akisoma ripoti ya vikundi hivyo Godfrey Makwinya ambaye ni katibu umoja wa walimu alisema madhumuni ya umoja huo ni kuviunganisha vikundi vya hisa vya wilaya hiyo ili umoja uweze kusimama na kuleta ufanisi katika vikundi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ujasiriamali na utunzaji wa kumbukumbu za fedha kwa wanachama wake na kutatua changamoto zinazowakabili katika biashara zao.
Makwinya alisema umoja huo una vikundi 48 ambavyo vimemaliza mzunguko wa mwaka wa kwanza vyenye wanachama 1294 kati ya hao wanaume ni 204 na wanawake 1090. Vikundi vimeweza kujiwekea akiba ya shilingi 187,842, 650/=, kugawana shilingi 235,653,730/= na kupata faida ya shilingi 47,811,080/=.
Alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni kutokuwa na vifa vya kutosha vya kuendesha ofisi vifaa hivyo ni samani za ofisi na Computer, wanahitaji msaada wa kitaalam ili waweze kufungua benki yao na uhaba wa fedha za kuendeshea shughuli za umoja wa walimu wa vikundi.
“Tunahakika kama malengo yetu yatakuwa kama tulivyopanga na baadhi ya changamoto zikatatuliwa, utakuwa umepunguza suala la umaskini kwa kiasi kikubwa kama si kuondoa kabisa katika wilaya yetu ya Nachingwea,” alisema Makwinya.
Kwa upande wa wanavikundi vya hisa ambao wamenufaika na mradi huo walimshukuru Mama Kikwete kwa kuanzisha mradi wa Mwanamke Mwezeshe na kuwapanua akili wanawake walioko vijijini ambao wamekopa fedha na kuzifanyia biashara na hivyo kujikwamua kiuchumi.
Zuhura Matola alisema, “Nilishindwa kusomesha watoto kwa kukosa ada, nikaamua kujiunga na vikundi vya hisa baada ya miezi minne ya kuweka akiba nikachukua mkopo na kuanzisha biashara ya kupika maandazi. Katika hela ya gawio nimefyatua matofali nataka kujenga nyumba ya kuishi.
“Hela ya gawio iliyobaki nimenunua vitenge ambavyo naviuza kwa kuwakopesha watu. Hivi sasa mimi na familia yangu tunakula, tunavaa na wanangu wanasoma bila ya matatizo hakika mradi huu umetusaidia sisi wanawake ambao uchumi wetu ulikuwa mdogo tumeweza kufanya mambo yetu wenyewe bila ya kuomba msaada wa kifedha kutoka sehemu ningine”.
Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi wa Mwanamke Mwezeshe ulishaunda vikundi 1,047 na kuwafikia wanavikundi 26,710 kati ya hivyo vikundi 438 viko wilaya ya Nachingwea na vina wanavikundi 11605.
Miongoni mwa shughuli za mradi ni kutoa mafunzo ya kuweka akiba ambayo yatawawezesha wanavikundi kuweka akiba za jumla ya shilingi bilioni moja na nusu kwa kipindi cha miaka mitatu ya mradi, kufikia mwishoni mwa mwaka jana mradi ulikusanya shilingi 1,518,643,430/= na hivyo kuvuka lengo la mwaka la kukusanya akiba ya shilingi milioni 500/=.