Na Mwandishi Wetu
Bagamoyo
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo, Magesa Mulongo, ameanza kupata vitisho kutoka kwa baadhi ya watumishi ambao ameagiza wakatwe mishahara kufidia fedha za miradi ya maendeleo ambazo zimeliwa chini ya usimamizi wao.
Mkuu huyo alisema hayo jana mjini hapa katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, na kuomba kamati hiyo isaidie ili walio kula fedha hizo wapate adhabu kali kwani wapo wanaolindwa na baadhi ya watu.
“Nimekuwa nikifuatilia juu ya wale walihusika na kutafuna fedha za miradi ya maendeleo, lakini nimejikuta nikitishiwa maisha, pia imefikia hatua hadi nataka kuwekewa sumu, kutokana na kusema ukweli juu ya miradi hiyo,” alisema.
Aliongeza kuwa, mbali na kupata vitisho, pia amefunguliwa kesi ya jinai katika Mahakama ya Wilaya Kibaha, hiyo yote ni kutaka kumnyamazisha asipambane na wale wahusika wa halamshauri hiyo waliokula fedha za miradi ya maendeleo.
Aidha alimuomba Kamimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Idd Azzan kufuhatilia suala hilo ili wale walikula fedha za miradi Bagamoyo, wachukuliwe hatua.
Alisema kingine ambacho kinamshangaza ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Roda Nsemwa kusimamishwa kazi, bila kutolewa kwenye nyumba ya Serikali jambo ambalo limefanya Mkurugenzi mpya, Samwel Saliyaga kuishi kwenye nyumba ya kupanga.
Aliongeza kuwa mbali na Mkurugenzi huyo kusimamishwa kazi ilitakiwa Serikali (TAMISEMI) inatakiwa imuondoe kwenye nyumba hiyo, lakini cha kushangaza hata barua tuliohoji juu ya suala hilo haijajibiwa.
Mkuu huyo aliongeza kuwa hata wafanyakazi waliopo katika halmashauri hiyo wanashindwa kufanya kazi na kuwa na wasiwasi hiyo yote inatokana na kufanyiwa vitisho na wale wanaowalinda walikula fedha za miradi hiyo.
Katika shughuli ya ukaguzi wa miradi kamati hiyo ilibaini dosari nyingi baada ya kukuta miradi mingi ikiwa imechakachuliwa.
Kaimu Mwenyekiti wa Kamati huyo alisema miradi mingi imeorodheshwa katika vitabu lakini hailingani na thamani ya fedha zilizotumika.
“Miradi mingi ni mibovu, fedha zinaonekana kutumika nyingi, lakini miradi haiendani na fedha hizo,” alisema Azzan.
Aliongeza kuwa, ukaguzi wa miradi hiyo umeonesha kuwa kuna upungufu mkubwa huku wahusika walioihujumu kuwa na kesi.
Alimwakikishia Mkuu wa Wilaya hiyo, kutoa ushirikiano na kamati yake ili kuhakikisha vitisho haviathiri athabu inayoendelea kwa wahujumu wilaya hiyo.