Waliokamatwa kwa Tuhuma za Kusambaza Matokeo ya Urais Mahakamani

Vijana waliokamatwa wakiwa katika mahakama hiyo.

Vijana waliokamatwa kwa tuhuma ya kusambaza matokeo ya urais wakiwa katika mahakama hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (katikati), akizungumza na mmoja kati ya vijana nane waliofikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa tuhuma za kusambaza matokeo ya kura za mgombea nafasi ya urais wa chama hicho katika mitandao ya kijamii kinyume na utaratibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Imedaiwa vijana zaidi ya 190 walikamatwa kwa kosa hilo.
 Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam leo.
Askari wa FFU wakiimarisha ulinzi mahakamani hapo.
Wafuasi wa Chadema wakionesha alama ya vidole viwili wanayoitumia.

 

Viongozi wa Chadema wakitoka katika mahakama hiyo baada ya kusikiliza kesi hiyo. 
 
Na Dotto Mwaibale
 
WATU wanane akiwemo Raia mmoja wa Korea na raia mmoja wa Kenya wamepandishwa kizimbani kwa kusambaza taarifa za matokeo ya urais katika Mtandao wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi yakiwa na kichwa ‘M4C election result management system’ bila kuthibitishwa kwa lengo la kupotosha umma. 
 
Sanjari na hilo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), amewasilisha mahakamani hati ya kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile alichadai kuwa ni kwa sababu ya usalama na kwa maslahi ya Taifa.
 
Washtakiwa hao ni Mashinda Mtei (49) mkazi wa Tengeru Arusha, Julius Mwita (40) mwanasiasa na ni mkazi wa Magomeni, Frederick Fussi (25) IT, mkazi wa Mbezi, Julius Matei (45) raia wa Kenya, Meshack Mlawa (25) mchungaji na ni mkazi wa Keko, Anisa Rulanyan (41) Mhandisi, mkazi wa Kawe, Jose Nimi (51) mkazi wa Uingereza na Kim Hyunwook (42) raia wa Korea.
 
Wakili wa Serikali Mkuu Edwin Kakolaki alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Respicius Mwaijage wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa washtakiwa wanashtakiwa kwa mashtaka matatu.
 
Ilidaiwa kuwa katika shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote, ambapo inadawa kati ya Oktoba 25 na 26 mwaka huu, wakiwa katika vituo tofauti tofauti ndani ya jiji la Dar es Salaam walitoa taarifa za uongo kwenye mitandao wakati wakijua hazijadhibitishwa.
 
Kakolaki alidai washtakiwa hao walisambaza taarifa hizo kwenye mtandao huo na katika mitandao mingine ya kijamii ambayo ni  Facebook na Twitter kutangaza matokeo ya urais ya mwaka huku kwa lengo la kuposha umma huku wakijua hayajadhibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
 
Katika shtaka la pili linamkabili Matei, Nimi na Hyunwook, ambapo wanashtakiwa kuwa Oktoba 26 mwaka huu wakiwa katika hoteli ya King iliyopo Kinondoni , Dar es Salaam wakiwa na hati za kusafirilia zenye namba A1532119, 930879 na M 27687807 walijiingiza katika ajira ya kukusanya na kusambaza matokeo ya urais ya uchaguzi wa mwaka huu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) bila kibali.
 
Pia, alidai katika shtaka la tatu lina mkabili Matei peke yake ambaye akiwa raia wa Kenya mwenye hati ya kusafirilia namba A1532119 akiwa ndani ya jiji  la Dar es Salaam alijihusisha na biashara katika Saccos ya Wanama bila kibali.
 
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka hayo, walikana kuhusika na tuhuma hizo, ambapo Kakolaki alidai upelelezi bado haujakamilika na pia alidai DPP amewasilisha hati ya kuzuia dhamana kwa sababu ya usalama na maslahi ya Serikali.
 
Wakili wa washtakiwa hao Peter Kibatala, alidai kuwa mashtaka yanayowakabili wateja wake yanadhaminika, kwa hiyo aliiomba mahakama iwapatie dhamana.
 
Pia, alidai hati hiyo ya DPP haiko mahakamani hapo kihali na kuiomba Mahakama itupilie mbali hati hiyo kwa sababu haina mashiko kisheria.
 
Kibatala alidai kuwa hati ya mashtaka iko tofauti na hati ya DPP kutokana na kifungu kilichokuwepo kuwa si sahihi, kwa hiyo kama ni hivyo hati hizo zote hazifai, kutokana na mapungufu hayo.
 
Baada ya Kibatala kudai hivyo, wakili Kakolaki alidai kuwa hati ya DPP ipo kihalali mahakamani na anayuetakiwa kuthibitisha hilo na mahakama kwa hiyo waiyachie mahakama.
 
Alidai kuhusu kifungu kilichotumika ni sahihi, akaiomba mahakama itupilie mbali hoja za Kibatala na washtakiwa wanyimwe dhamana kwa mujibu wa sheria, baada ya DPP kuwasilisha hati hiyo.
 
Hakimu Mwaijage alisema uamuzi wa hoja hizo atazitoa Oktoba 30 mwaka huu na washtakiwa aliamuru warudishwe rumande.
 
Nje ya mahakama
 
Washtakiwa hao waliondoka katika eneo hilo la mahakama wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi ambapo wakiwa ndani ya magari ya polisi walikuwa wakionesha alama za vidole viwili.
 
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sauti, Profesa Mwasiga Baregu na viongozi wengine wa Chadema walijitokeza mahakamani hapo kufuatilia shauri hilo.(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)