Na Shomari Binda, wa Binda News, Musoma
BAADA ya kuitikisa nchi kwa mgomo wa siku nne hatimaye walimu wa shule mbalimbali za msingi na Sekondari mjini Musoma wamerejea kazini baada ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kudai kuwa mgomo huo ulikuwa batili na haukuzingatia matakwa ya kifungu cha 84 (1) (2) cha sheria ya ajira ma mahusiano kazini ya mwaka 2004 na kudai kuwa uliandaliwa kwa dhamira mbaya.
Mwandishi wa habari hii alitembelea shule mbalimbali za Manispaa ya Musoma na kuwashuhudia walimu wakiwa madarasani wakiendelea na kazi huku wakikataa kuzungumzia suala hilo kwa kuwa tayari liko mahakamani.
Walimu katika shule ya msingi Mukendo wakiwa zaidi ya watano walikuwa katika jengo la darasa la saba wakifanya kazi ya kuwajazia wanafunzia wanaotarajiwa kumaliza elimu ya msingi fomu za PSLE. Walisema kuwa wameamua kuzijaza fomu hizo kwa kushirikiana kwa pamoja ili kuweza kuzikamilisha kwa haraka kutokana na muda wa kuziwakilisha katika Baraza la Mitihani la Taifa ukiwa unakaribia kuisha.
Mmoja wa walimu hao aliyejitambulisha kwa jina la Justine Harrison alisema kutokana na shule kufungwa wameamua kushirikiana ili kulikamilisha zoezi hilo la ujazaji wa fomu ili waweze kuzituma mahala panapo husika kwa wakati.
Alisema kuwa kutokana na fomu hizo kutakiwa kujazwa kwa umakini mkubwa ndiko kulikopelekea walimu wengi kushiriki kuifanya kazi hiyo ili kila mwanafunzi ajaziwe taarifa zake zilizo sahihi ili kuepusha kasoro ambazo zinaweza kujitokeza kipindi cha mitihani ya mwisho.
Katika upande wa shule ya msingi Mwembeni BINDA NEWS ilikutana baadhi ya wanafunzia wa darasa la nne wakiwa wanarudi nyumbani kabla ya shule kufungw wakidai kuwa hawakufanya mitihani ya majaribio kwa ajili ya kufunga muhula huo hivyo wameamua kurudi nyumbani. Katibu wa Chama cha Walimu Mkoa wa Mara Fatuma Bakari hakuweza kupatikana Ofisini kwake wala kwenye simu yake ya mkononi ili aweze kuzungumzia marejeo ya walimu mashuleni katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mara.
Katika mahamuzi ya Mahakama Jaji wa Mahakama kuu Divisheni ya kazi Sophia Wambura katika maamuzi yake hapo jana alasiri aliwataka walimu wote waliogoma kurejea kazini mara moja kuendelea na kazi.
Alisisitiza kuwa CWT imeitisha mgomo huo ikiwa na dhamira mbaya kwa sababu wao ndiyo waliokataa kuendelea na mazungumzo na mwajiri wake na badala yake wakaanzisha mgomo ulioanza Julai 27.