Yohane Gervas, Rombo
WALIMU wawili wa Shule ya Sekondari Ubaa iliyopo katika tarafa ya Mkuu Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wanatuhumiwa kumshambulia na kumjeruhi vibaya kwa fimbo mwanafunzi wa kidato cha nne, Loveness Minja kwa kile kinachodaiwa kuwa alikataa kulipa shilingi 2,500 kwa ajili ya sherehe ya kuwakaribisha wanafunzi wa kidato cha kwanza (welcome form one).
Mkuu wa shule hiyo, Alphonce Shao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema kuwa lilitokea Februari 28 mwaka huu na wanaodaiwa kuhusika ni mwalimu Eunice Minja, ambaye pia ni dada wa mwanafunzi aliyejeruhiwa na mwalimu mwingine alimtaja kuwa ni Mgonja.
Akizungumza Mkuu huyo wa shule alisema hana uhakika kwamba wanaotuhumiwa walitenda kosa hilo kama inavyodaiwa na mwanafunzi huyo. Alisema mwanafunzi huyo alilazwa katika Hospitali ya Huruma kwa muda wa siku tano kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo mgongoni, mikononi pamoja na sehemu za mabegani.
Mwalimu Shao alisema ni mapema kuthibitisha kuwa mwanafunzi huyo alipewa adhabu hiyo kwa kile kushindwa kulipia hela ya sherehe kwani kama inavyodaiwa kwani wapo wanafunzi wengine ambao nao hawakulipa hela hiyo na hakuna aliepewa adhabu.
Alisema bado anafuatilia kwa kuwahoji wahusika ili kujua chanzo halisi na kusisitiza kuwa adhabu hiyo haina uhusiano na adhabu za shule kwani taarifa za awali zinaonesha wahusika walikuwa na ugomvi wao mwingine na kipigo hicho hakina uhusiano na masuala ya shule.
Hata hivyo kwa upande wao waalimu wanaohusishwa na tukio hilo wakizungumza na mtandao huu (Mwalimu Mgonja) alisema ni kweli alimchapa mwanafunzi huyo viboko vitatu kama mlezi wake wa kike kwa kushindwa kulipa mchango wa sherehe ya ukaribisho kidato cha pili na baadaye alimwacha akiwa na dada yake ambaye ni mwalimu Eunice Minja.
Minja alipoulizwa kama utaratibu unaruhusu kuwaadhibu wanafunzi wasiolipa michango ya sherehe kama hizo alikiri kuwa utaratibu hauruhusu ila alimpa adhabu hiyo kwa kuwa mwanafunzi huyo alikataa kumwomba dada yake hela ya sherehe.
Kwa upande wake mwalimu Eunice Minja ambaye pia anatuhumiwa alisema kuwa alimshughulikia kama mzazi kwa kukataa kuomba hela na akasema kuwa utaratibu unaruhusu kufanya hivyo na alipotakiwa kutoa ufafanuzi zaidi aligoma kwa kudai kuwa yeye si msemaji wa shule.
Inadaiwa kuwa baada ya mwanafunzi huyo kupata kipigo hicho alifukuzwa nyumbani na wakati akiondoka alikimbia na kuanguka karibu na eneo la mahakama ya mwanzo Ubaa baada ya kuishiwa nguvu, ndipo wasamaria walimsaidia kwa kumpatia huduma ya kwanza na kisha kupiga simu polisi kuomba msaada kabla ya kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.