Walimu 81 wakacha kuripoti Rukwa

Na Mwandishi Wetu
Sumbawanga

ZAIDI ya walimu 81 waliopangiwa kufundisha shule mbalimbali za sekondari zilizopo mkoani Rukwa hawajaripoti katika vituo vyao vya kazi, limefahamika.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini hapa Ofisa Elimu, Taaluma Mkoa wa Rukwa, Albert Mloka alisema walimu hao ni kati ya walimu 303 waliopangiwa na Serikali mwezi Januari mwaka huu kufuatia mkoa huo kuwa na uhaba wa walimu kweny shule anuai.

Alisema kati ya walimu waliopangiwa wapo walimu wa shahada 176 na stashahada ni 127, lakini walioripoti ni 222 ikiwa ni sawa na asilimia 73.3, wengine waliobakia wakishindwa kuripoti pasipo na sababu za msingi, huku nyingi zikielezwa ni mazingira magumu ya kazi.

Mkoa huo una shule za sekondari 99 hivyo bado kuna mahitaji makubwa ya walimu, hasa kwenye za sekondari za kata ambazo baadhi yake zina walimu watatu tu hivyo kushindwa kutimiza mahitaji ya wanafunzi ya kupata elimu bora.

Katika hatua nyingine, Mloka alisema kuwa licha ya agizo lililowahi kutololewa na Kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) juu ya umuhimu wa utoaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi, lakini shule nyingi za msingi na sekondari mkoani Rukwa hazijatekeleza agizo hilo.

Alisema kila halmashauri ya wilaya imekuwa ikitoa sababu zake zinazokwamisha agizo la utoaji wa chakula shuleni, ambapo kati ya idadi ya shule za msingi na sekondari 607 zinazotoa chakula za msingi ni 95 tu huku za sekondari ni 30.

Alizishauri halmashauri za wilaya, miji na manispaa kuhimiza suala la utoaji wa chakula shuleni kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza utoro shuleni na hatimaye kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya mwisho.