Na Mwandishi Wetu
VIKWAZO kadhaa vinavyowakabili watu wenye ulemavu hasa kupata elimu na ufahamu wa kutosha juu ya ugonjwa wa Ukimwi, vinairudisha nyuma jamii hiyo. Walemavu hawa wamekuwa wakishindwa kupata huduma za kijamii zikiwemo za ushauri na elimu kuhusu maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi.
Vikwazo vingine ni pamoja na kukosekana kwa miundombinu stahili kwa jamii husika pamoja na imani potofu kwa juu ya watu wenye ulemavu.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam wakati wa kuhitimisha miaka mitatu ya Mradi wa uelimishaji ukimwi kwa watu wenye ulemavu, ambao umeratibiwa na Hospitali ya CCBRT na kufadhiliwa na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa ukimwi (PEPFAR).
Meneja wa Mradi huo, Clement Ndahani alisema walemavu wa macho wanashindwa kusoma maandiko kuhusu maambukizi ya ukimwi pamoja na elimu kuhusu ugonjwa huo na kusisitiza juu matumizi ya maandishi maalumu ya wasioona.
Ndahani alisema CCBRT wameanzisha mtaala wa masomo ya wakalimani wa viziwi amao utawawezesha kufundisha watoa ushauri nasaha na watoa huduma hospitalini ili waweze kutoa huduma hiyo kwa watu wa aina hii.
Alisema viziwi wengi wanashindwa kupata elimu hii kwa sababu wanakosa mawasiliano ya lugha baina yao na watoa huduma hao ambapo hutumia lugha ya ishara inayohitaji utaalamu.
Ndahani alibainisha kuwa fikra potofu kuwa walemavu wapo salama zimekwamisha juhudi za kupunguza kasi ya maambukizi kwa kuwa watu wamekuwa wakishiriki na walemavu katika vitendo hatarishi.
Alisema CCBRT kwa ushirikiano na Tume ya Kudhibiti Ukimwi(Tacaids) ilifanya utafiti na kubaini kundi la walemavu lipo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi hivyo wanaongeza ufahamu kwa kundi hili.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Erwin Telemans alisema wameweza kuwafikia Watanzania 45,000 ambao wengi wao ni walemavu na kuwapa elimu juu ya janga hilo na aliishukuru Wizara ya Afya na Utawi wa Jamii kwa kushirikian nao katikakufanikisha hili.
Telemans aliwataka wadau mbalimbali kuungana na kufanya miradi mingine ya kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa wengi wao wanasahaulika na kutopata elimu ya ukimwi hivyo kuweza kujikinga.
Alisema katika mradi huo wameweza kufikia wilaya 15 na nyingi kati ya hizo zipo maeneo ya mbali yasiyoweza kufikiwa kwa urahisi hivyo kuhakikisha wanayafikia.