Walemavu wa Viungo Wafarijiwa na Mke wa Rais

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimkabidhi Kiongozi wa Kituo cha walemavu cha Raisbura Bwana Mohamed Chitawala baadhi ya vyakula alivyowaletea- mchele, unga, mafuta ya kupikia, sukai, soda na vinginevyo wakati alipotembelea kituo cha walemavu cha Rasibura huko Lindi siku ya Pasaka tarehe 20.4.2014. Picha na John Lukuwi.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akimkabidhi Kiongozi wa Kituo cha walemavu cha Raisbura Bwana Mohamed Chitawala baadhi ya vyakula alivyowaletea- mchele, unga, mafuta ya kupikia, sukai, soda na vinginevyo wakati alipotembelea kituo cha walemavu cha Rasibura huko Lindi siku ya Pasaka tarehe 20.4.2014. Picha na John Lukuwi.

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

WATU wenye ulemavu wa viungo wametakiwa kutosikitika kwanini Mwenyezi Mungu aliwaumba hivyo na kujiona wanyonge bali wajione wako sawa na watu wengine kwani katika maisha ya binadamu kila jambo lina makusudi yake. Hayo yamesemwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wazee wenye mahitaji maalum wanaoishi katika kituo cha Rasbura kilichopo wilaya ya Lindi mjini.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alifika kituoni hapo kwa ajili ya kuwajulia hali wazee hao na kuwapatia zawadi mbalimbali za mchele, nyama, sukari, unga wa ugali, vitunguu, mafuta ya kupikia, nyanya na soda kwa ajili ya sikukuu ya Pasaka.

Alisema inawezekana Mwenyezi Mungu aliwaumba hivyo walivyo ikiwa ni kwa makusudi ili iwe njia rahisi ya kumfikia yeye na kuwataka kushukuru kwa yote. Jambo la muhimu aliwaomba waendelee  kuishi kwa amani na upendo kama ndugu.

“Nilipanga siku ya leo kusherehekea sikukuu ya Pasaka pamoja nanyi huwa nafanya hivi katika sikukuu mbalimbali kama X-Mass na Mwaka mpya, nasherehekea na watoto yatima na watu wazima wa dini mbalimbali nawaomba adhimisheni siku hii katika mazingira ya upendo, amani na utulivu”, alisema Mwenyekiti huyo wa WAMA.

Akielezea Historia ya kituo hicho kinachomilikiwa na kanisa Katoliki Jimbo la Lindi Mkurugenzi wa KARTAS Mzee Saimoni Mnimbo alisema miaka ya nyuma kituo hicho kilikuwa ni Gereza la wafungwa lakini mara baada ya kujengwa kwa gereza jipya ndipo Serikali ililipatia jengo hilo Idara ya Ustawi wa jamii na ikaanza kulitumia kama kituo cha wazee wasiojiweza.

Mzee Mnimbo alimshukuru Mama Kikwete kwa moyo wake wa huruma na kuamua kwenda kuwatembelea na kuwapatia zawadi mbalimbali vikiwemo vyakula na vinywaji na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano ingawa kanisa linawahudumia wazee hao bali nao wanatakiwa kuwasaidia.

“Tunawashukuru wadau mbalimbali wanaotuunga mkono na kuwahudumia wazee hawa. Hapa kwetu hakuna  tatizo la maji, kuna kipindi mji mzima wa Lindi haukuwa na maji lakini katika kituo hiki tulikuwa na maji ya kutosha tunaishukuru ofisi ya Mkuu wa mkoa kwa kutulipia bili ya maji kila mwezi,” alisema Mzee Mnimbo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi Mzee Ally Mtopa alisema katika kituo hicho hakuna mambo ya udini kwani binadamu wote ni sawa na kwa yeyote anayejijuwa kuwa yeye ni binadamu basi akili yake ikitazame kituo hicho na kuweza kukisaidia .

Naye Mzee Mohamed Chitawala ambaye anaishi katika kituo hicho alisema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za afya kwani wakienda Hospitali kupata matibabu wanapata usumbufu na katika kituo hicho hakuna dawa za huduma ya kwanza.

Tangu mwaka 1995 kituo hicho kinamilikiwa na kanisa Katoliki jimbo la Lindi, wazee wanaoishi hapo wana ulemavu wa macho na viungo kutoka dini zote ambao wametelekezwa na jamaa zao. Idadi yao ni 10 kati yao wanawake ni sita na wanaume ni wanne kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huu.