Wakuu wa Tume za Uchaguzi EAC Waishauri Tume ya Uchaguzi Kenya

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi Kenya Bw. Ahmed Issack Hassan

Na Mark Mugisha, EANA-Arusha

WAKUU wa tume za uchaguzi kutoka nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameishauri Tume Huru ya Uchaguzi nchini Kenya (IEBC) kuzingatia misingi imara ya demokrasia katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Machi,2013.

Wakuu wa tume za uchaguzi za EAC wanakutana mjini Nairobi, Kenya, kutathmini mapendekezo ya mswada wa Usimamizi wa Uchaguzi na Ufanyaji Tathmini katika nchi wananchama za EAC. Iwapo mswada huo utaridhiwa na EAC wiki ijayo, Kenya itakuwa nchi ya kwanza kunufaika na mpango huo.

“Changamoto zipo nyingi lakini tuna uhakika kwamba uchaguzi wa Kenya utafanikiwa ipasavyo,” wajumbe wa mkutano huo waliliambia Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) kwa nyakati tofauti.

Wajumbe pia waliutaka uchaguzi huo wa Kenya uwe wa amani, wakifafanua kwamba kufanyika kwa amani kwa uchaguzi huo, kutakuwa ni mfano mzuri kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki. Hata hivyo, Mkuu wa Ujummbe wa Burundi, Balozi Pierre Clavier alitoa wito kwa vyama vya siasa kuonyesha kuvumiliana wakati wa mwenendo mzima wa uchaguzi na utangazaji wa matokeo.

“Demokrasia inapata matatizo kutokana na viongozi wa vyama vya siasa kutokuwa tayari kukubali ushindani wa kisiasa,” aliowaambia wajumbe wa mkutano huo wakiwemo, wasajili wa vyama vya siasa, wanasheria, wanaharakati, wataalamu wa masuala ya haki za binadamu, waandishi wa habari na watunga sera wa serikali.

Naye mjumbe kutoka Rwanda, Charles Munyaneza alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa waangalizi wa masuala ya uchaguzi wa muda mrefu ili kuweza kutoa tathmini ya kina katika uchaguzi. Alipendekeza pia kuwepo na ufadhili wa ndani wa masuala ya uchaguzi ili kuweza kudhibiti mwenendo mzima wa uchaguzi inavyotakiwa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa EAC, anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Dk. Julius Rotich alisema Kenya haina budu kuchukua hatua zote muhimu kukwepa maafa yaliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwaka 2007. Baada ya uchaguzi huo kulitokea ghasia zilizosimamisha operesheni zote nchini humo pamoja na biashara ndani ya kanda ya Afrika Mashariki.

Ofisa huyo mwandamizi wa EAC aliwakumubusha wajumbe kwamba pindi mswada huo wa usimamizi wa uchaguzi ukifikiriwa na hatimaye kupitishwa,utakuwa ni chombo cha kuongoza chaguzi mbalimbali ndani ya kanda ya EAC.

Naye mwenyekiti wa mkutano huo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa IEBC, Lilian Mahiri-Zaja alisema nchi yake sasa inafanyakazi kwa kufuata misingi ya katiba mpya na uchaguzi wa mwaka ujao utakuwa mtihani mkubwa kwa demokrasia nchini humo.