Wakuu wa Nchi SADC Kumthibitisha Mtanzania Kuwa Katibu Mtendaji

Wakuu wa Nchi SADC Kumthibitisha Mtanzania Kuwa Katibu Mtendaji

WAKUU wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Agosti 17, 2013, wanatarajiwa kumdhibitisha Dk. Stergomena Tax wa Tanzania kuwa Katibu Mtendaji mpya wa SADC.

Dk. Tax ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki amependekezwa na Baraza la Mawaziri la SADC kuwa Katibu Mtendaji mpya kuchukua nafasi ya Dk. Tomaz Augusto Salamao ambaye amemaliza muda wake wa utumishi wa Jumuia hiyo. Dk. Tax amependekezwa na Baraza la Mawaziri la SADC kuwa Katibu Mtendaji mpya kufuatia uchaguzi wa nafasi hiyo uliofanywa na Baraza hilo.

Katika uchaguzi, Dk. Tax alipata wastani wa alama 79 wakati mpinzani wake, Mheshimiwa Peter G. Sinon, Waziri wa Serikali ya Shelisheli amepata wastani wa alama 72. Sinon ni Waziri wa Uwekezaji, Raslimali na Viwanda wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Mkataba wa Kuanzishwa kwa SADC, Katibu Mtendaji wa Jumuia hiyo hupendekezwa na Baraza la Mawaziri na huthibitishwa na Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuia hiyo. Dk. Salamao amekuwa Katibu Mkuu wa SADC kwa miaka minane iliyopita baada ya kuwa ametumikia vipindi viwili vya miaka minne kila kipindi na kwa mujibu wa Mkataba wa SADC hawezi kuendelea kushika nafasi hiyo.

Pamoja na Dk. Salamao, Naibu Katibu Mtendaji wa Jumuia hiyo kwa miaka minne iliyopita, Injinia Joao Samuel Caholo pia amemaliza muda wake. Hata hivyo, kwa sababu za kiufundi, nafasi yake haitaweza kujazwa kwenye mkutano wa sasa wa Jumuia hiyo.