Na Janeth Mushi, Arusha
WAFUGAJI na wakulima nchini wametakiwa kufufanya shughuli zao kwa kufuata ushauri wanaopatiwa na wataalamu ili kuongeza uzalishaji pamoja na ubora wa bidhaa wanazozalisha.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mtaalamu wa Pembejeo za Kilimo na Dawa za Mifugo, kutoka kampuni ya Keenfeeder’s wasambazaji wa dawa za mifugo na kilimo, Anzamen Muro alipokuwa akizungumza na wakulima katika maonesho ya Wakulima, Nane Nane yanayofanyika katika viwanja vya Themi Njiro mkoani hapa.
“Iwapo mtafuata na kuzingatia ushauri mnaopewa na wataalamu mtaweza kuongeza kasi ya uzalishaji pamoja na kuzalisha bidhaa zenye ubora zitakazowawezesha kupata masoko ya uhakika ,”alisema Muro
Mtaalamu huyo alisema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wataalamu wa mifugo hapa nchini ni pamoja na uelewa mdogo walio nao wafugaji hali inayowalazimu kufanya semina kwa ajili ya mafunzo kwa wakulima kwa kushirikiana na mashirika binafsi.
“Wafugaji wengi hapa nchini hufuga tu bila kutumia mbinu za kitaalamu hivyo kufuga kwa hasara bila tija hivyo tunalazimika kutoa elimu ili waweze kuondokana na ufugaji huo ambao unawagharimu bila kuwa na faida,” alisema Muro.
Aidha Mtaalamu huyo wa Kampuni ya Keenfeeder’s ya usambazaji wa madawa ya mifugo na kilimo, alisema kuwa wameanzisha kitengo maalum cha wataalam kwa ajili ya kuwapatia wafugaji na wakulima mafunzo.
Muro alisema timu hiyo itajikita zaidi kwa wafugaji na wakulima
waishio maeneo ya vijijini ili kuweza kuboresha uzalishaji na
kujiongezea kipato.
“Tunahakiksiha kuwa elimu hiyo inawafikia wakulima na wafugaji maeneo yote nchini kwa sasa tumeanza na maeneo ya Kanda ya Kaskazini lengo likiwa ni kumwinua mkulima na mfugaji ili aweze kuongeza uzalishaji na kipato,” alifafanua
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni huyo akizungumza na gazeti hili alisema kuwa kwa wakulima na wafugaji wa maeneo ya Kanda ya Kaskazini ambao tayari wameshapatiwa mafunzo hayo kiwango cha uzalishaji kimepanda tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya kuanza kutumia njia za kitaalamu.
Akizungumzia suala la ukosefu wa madawa kwa ajili ya mifugo hususani madini, alisema mwaka 2006 walifanya utafiti na kugundua madini ya (calcium Phosphorus) aina ya Ng’ombe Mix na kuanza kuyazalisha ambapo wafugaji wameweza kuondokana na magonjwa ya ukosefu wa Calcium yaliyokuwa yanaikabili mifugo mingi.
Amewataka wakulima na wafugaji kuzingatia ushauri wa kitaalamu na
kujitokeza katika mafunzo mbalimbali ya kitaalam yanayokuwa yakitolewa na wataalamu hapa nchini.