KILIO cha wakulima tumbaku kuhusiana ukosefu wa soko pamoja na bei kubadilika kitamalizwa hivi karibuni baada ya zao hilo kupata kibali cha kuuzwa kwenye soko la China. Hayo yamebainika Oktoba 18, 2013 wakati Makamu Rais wa Bodi ya Tumbaku ya China, Bw. Yang Peisen alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika nyumba ya wageni ya Serikali ya Diaoyutai jijini Beijing, China. Bodi hiyo ya Tumbaku (State Monopoly Tobacco Administration – STMA) ndicho chombo cha juu cha maamuzi kuhusiana na zao hilo.
Akizungumza na Bw. Peisen na msafara wake pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania alioambatana nao, Waziri Mkuu aliwasihi waangalie uwezekano wa wafanyabiashara wa China kujenga kiwanda cha kutengeneza bidhaa za tumbaku katika maeneo ya Songea na Tabora ambako Tumbaku inalimwa kwa wingi ili kuwasaidia wakulima wa maeneo hayo na mikoa ya jirani.
“Ndoto yangu ni kuona kampuni za China zinakuja kujenga kiwanda Tanzania, mkilifanya hili mtakuwa mmetusaidia sana kuondoa umaskini miongoni mwa wakulima na utakuwa ndiyo ukombozi kwa wakulima wetu,” alisema Pinda.
Alisema sasa hivi kuna kiwanda kimoja tu cha kutengeneza sigara ambacho kiko Dar es Salaam na kwamba mahitaji ya kiwanda ni madogo kuliko kiasi cha tumbaku inayozalishwa nchini hali inayowafanya wakulima wahangaike kutafuta masoko.
Kwa upande wake, Bw. Peisen alisema vikwazo vya kiufundi ambavyo vilikuwa vikizuia tumbaku ya Tanzania isiingie katika soko la China hivi sasa havipo kwani mwaka jana walituma timu ya wataaalamu kuja Tanzania ili kupata sampuli za tumbaku na kuangalia jinsi zao hilo linavyopakiwa (packaging). Alisisitiza haja ya zao hilo kuwa na ubora unaostahili ili liweze kupata soko katika nchi hiyo.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku Tanzania, Bw. Wilfred Mushi ambaye yuko kwenye msafara wa Waziri Mkuu, alimhakikishia Bw. Peisen suala la ubora wa tumbaku na kusisitiza kuwa soko la China ni muhimu kwa Tanzania kwani kwa sasa wanauza katika nchi za Ulaya tu na wakati mwingine soko la huko linayumba na hivyo kumwingizia hasara mkulima.
Alisema China ni taifa linalolima kwa wingi tumbaku; lakini pia watu wake wanavuta sana sigara hivyo bado wanahitaji bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi. “Tukipata soko la China kutakuwa na ushindani wa magharibi na mashariki na wakulima wetu watapata bei nzuri,” alisema Bw. Mushi.
Alisema makampuni matatu kutoka Tanzania yalishajaribu kuomba kuuza bidhaa hiyo nchini China lakini yaligonga mwamba kutokana na ukiritimba ambao STMA ilikuwa imeweka. Aliyataja makampuni hayo kuwa ni Tanzania Tobacco Leaf Company (TLTC), Alliance One na Premium America.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.
Pia amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye.