Wakulima wa Mpunga Walalamikia Ukosefu wa Pembejeo Kaskazini Unguja

WANANCHI wametakiwa kuendelea kuiamini Serikali na viongozi wake na kuepuka kulaumiana badala yake kushikamana katika kukabiliana na changamoto za maendeleo zinazolikabili taifa.

Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati alipokuwa akizungumza na wakulima wa bonde la Kilombero huko Mwembe Mpunga wilaya ya Kaskazini ‘B’ mkoa wa Kaskazini Unguja.
Rais alifika katika bonde hilo kukagua athari za jua kwa kilimo cha mpunga katika bonde hilo katika siku yake ya pili ya ziara ya siku mbili kutembelea mkoa huo.

Katika maelezo yao kwa Rais wakulima hao walieleza kutoridhishwa na kiwango kidogo cha madawa ya kuulia magugu wanachopewa, huduma hafifu za matrekta na kutokupatikana kwa wakati mbegu za muda mfupi“Tuwe na subira…tusinune wala tusimchukie mtu…tusilaumiane kwani lawama hazijengi na kulaumiana ni ishara ya kutoaminiana na hicho si kitu kizuri. Wenzetu (watendaji) wanafanya kazi nzuri lakini sikatai kuwa wapo wanaofanya makosa lakini hilo liko kwa kila binadamu wote” alisema Dk.Shein.

Aliwahakikishia wananchi hao kuwa azma na dhamira ya serikali ya kufanya mapinduzi ya kilimo ni thabiti na imeanza kutekelezwa kwa vitendo ambapo hatua mbalimbali zimechukuliwa kutekeleza azma hiyo.“tuahidi kutoa ruzuku ya mbegu, mbolea na madawa ya kuulia magugu tena ruzuku ya kiwango kubwa ya asilimia 75 ya vitu hivyo huku nyinyi mkilipia asilimia 25 tu.Tumeleta pia matrekta. Katika kipindi hiki cha miaka miwili tumeongeza kiwango cha mahitaji ya wakulima na hayo ni maamuzi makubwa ya Serikali yenu” Dk. Shein aliwaambia wakulima hao na kusisitiza kuwa hatua hizo ni ishara tosha ya dhamira ya kweli ya Serikali kutekeleza ahadi yake kwao.

Wakati huo huo Serikali imesema haiwezi kuagiza kiwango kikubwa cha madawa ya kuulia magugu kwa wakati mmoja kulingana na mahitaji ya wakulima kutokana na kuchelea uharibifu wa mazingira ambao unaweza kusababishwa na matumizi ya madawa hayo kupita viwango vinavyokubalika kimataifa.

Akitoa ufafanuzi kwa wakulima wa Bonde la Kilombero ambao walilalamikia kiwango kidogo wanachopewa cha madawa hayo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Ndg. Affan Othman aliwaeleza wakulima hao mbele ya Rais kuwa ni kweli madawa yaliyopo hivi sasa hayatoshelezi mahitaji ya wakulima lakini kiwango kilichopo kimezingatia athari za matumizi ya madawa hayo kwa mazingira.“Ni kweli kuwa kiwango cha madawa ya kuulia magugu tulichonacho hakitoshelezi mahitaji ya wakulima kwa sasa ambacho ni lita karibu 100,200 lakini usambazaji wa madawa haya unazingatia viwango vinavyokubalika kimataifa cha matumizi ya madawa hayo kwa kila nchi”alifafanua.

Katibu Mkuu huyo alieleza kuwa madawa hayo ni sumu na yanapotumika huingia ardhini na hatimae kuchanganyika na maji ambapo kiwango kikizidi huathiri maji na hatimae afya za watu watakaotumia maji hayo na ndio maana kila nchi imepewa kiwango chake cha matimizi ya madawa hayo.

Kuhusu mgawanyo wa madawa (na pembejeo nyingine za kilimo kama mbegu na mbolea) Ndg. Affan alisema jukumu hilo hufanywa kwa ushirikiano kati ya wizara yake na jumuiya za wakulima katika maeneo husika.“Ni kweli matrekta tuliyo nayo hayatoshi lakini tumo mbioni kukunua mengine, mbegu za muda mfupi zipo lakini nasaha zangu kwa wakulima wafuate maelekezo ya wataalamu wetu na mashine za kuvunia tulizonazo hazitoshi lakini tumeshaagiza nyigine 10 kutoka SUMA–JKT na mbolea ipo ya kutosha na baadhi ya maeneo imebaki” alisema Katibu Mkuu huyo.

Katika ziara hiyo ya wilaya ya Kaskazini ‘B’ Rais alifungua rasmi skuli ya msingi ya Matetema, alikagua ufugaji wa kisasa wa ngombe wa maziwa huko Zingwezingwe na baadae kuzungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Kaskazini huko kwenye hoteli ya Sea Cliff ikiwa ni majumuisho ya ziara yake Mkoani humo.

Dk Shein anatarajiwa kuendelea na ziara yake kisiwani Pemba hapo kesho ambapo atakagua na kufungua miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ya serikali, binafsi pamoja na vikundi vya wajasiriamali.