Yohane Gervas, Rombo
WAKULIMA wa Kahawa Wilaya ya Rombo wametakiwa kutokata tamaa kulima zao hilo licha ya uwepo wa changamoto kadhaa katika uzalishaji wa zao hilo. Wakizungumza na wakulima na wadau wa zao la kahawa wamesema kuwa kilimo cha zao la kahawa kwa sasa kimedorora sana katika maeneo mbalimbali hapa nchini kutokana na wakulima kukata tamaa na kubadilisha matumizi ya mashamba ya kahawa kwa kupanda mazao mengine.
Akizungumza mmoja wa wadau wa zao hilo, Pius Kiwango (80) alisema kuwa bei ya zao la kahawa imeshuka sana kwa sasa hali inayochangia wakulima wengi kukata tamaa. Pia alisema hali hiyo inasababisha umaskini katika familia nyingi.
Aidha Kiwango alisema kuwa miaka ya nyuma walikuwa wakitegemea zao la kahawa kusomesha watoto, kuendeshea familia zao na hata kujengea na hivyo akasema kuwa endapo kilimo hicho kitaendelezwa vizuri hali ya umasikini katika wilaya ya Rombo itapungua. Pia amesema ipo haja ya Serikali kutumia wataalamu wake kutoa elimu vijijini ili wakulima wasiendelee kung’oa miti ya kahawa.
Wakati huo huo; imeelezwa kuwa ukosefu wa elimu ya utunzaji wa mazigira na uelewa mdogo wa wananchi juu ya sheria za utunzaji wa mazingira ndio kikwazo kikubwa kinachofanya kukwama kwa mpango wa utekelezaji wa utunzaji mazingira katika wilaya ya Rombo.
Kauli hiyo imetolewa na baadhi ya wananchi wakazi wa Rombo walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti wamefafanua kuwa wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira hali ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira katika maeneo wanayoishi.
Mmoja wa wakazi wa Rombo, Denis Silayo amesema iwapo wananchi watapewa elimu
ya kutosha juu ya umuhimu wa kutunnza na kuhifadhi mazingira itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazingira wilayani hapa.
Silayo aliongeza kuwa operesheni ya kuzuia ukataji wa miti wilayani hapa imeonekana
kusuasua kutokana na wananchi kutokuwa na elimu juu ya umuhimu wa kutunza mazingira.
Alisema licha ya Serikali kuwatumia viongozi wa vijiji na kata kutoa elimu ya mazingira bado kuna changamoto.
Aidha wametoa ushauri kwa serikali kutoa elimu ya mazingira kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi sekondari ili wanafunzi hao waitumie elimu hiyo pindi wanapokuwa mitaani. “…Wanafunzi wakipewa elimu hiyo watakua mabalozi wazuri wa kuhamasisha umuhimu wa utunzaji wa mazingira katika jamii.” alisema.