Wakulima wa Chai Korogwe Walilia Kiwanda cha Chai cha Wakulima

Baadhi ya mashamba ya zao la Chai Korogwe Vijijini

Na Joachim Mushi, Korogwe

WAKULIMA wa zao la chai wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga wameiomba Serikali kukubali kutoa eneo la ardhi ili wajenge kiwanda cha wakulima wa zao hilo kitakacho wasaidia wakulima kukuza thanani ya zao lao.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, hivi karibuni kijijini Bungu, Katibu wa Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Chai, Moses Sangoti alisema tayari wamempata muwekezaji ambaye amekubali kuwajengea kiwanda cha chai eneo la Sakare-Bungu, Korogwe Vijijini.

Sangoti alisema kujengwa kwa kiwanda hicho kutakuwa mkombozi kwa wakulima wa chai vijiji mbalimbali ambao wamekuwa wakiuza chai yao kwa bei ambayo haikidhi gharama za uzalishaji kwa mkulima.
Alisema juhudi za kuomba eneo la kujengwa kwa kiwanda hicho zimesha anza kwa kufikisha ombi lao kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga lakini bado hazijazaa matunda.

“Tumesha peleka ombi letu kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga, kwamba tunaomba Serikali ifute hati ya umiliki wa eneo linalotakiwa kujengwa kiwanda ambalo lilikuwa likimilikiwa na muwekezaji wa zamani (Humphrey Law) ili tujengewe kiwanda cha wakulima,” alisema Katibu huyo.

Aliongeza kwa sasa kilo moja ya zao la chai inanunuliwa kwa sh. 200 kutoka kwa mkulima na muwekezaji mmoja bei ambayo haikidhi gharama za uzalishaji, hivyo kuiomba Serikali iwakumbuke kwa kuharakisha mchakato huo wa kutoa eneo ili kijengwe kiwanda cha wakulima.