MKUTANO wa maafisa waandamizi kutoka Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi wa kuharakisha Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki umekubaliana kuanza kuandaa rasimu ya katiba ya shirikisho hilo.
Kama ilivyokuwa kwa timu ya wataalamu walioandaa Itifaki ya Soko la Pamoja, timu ya kuaada rasimu ya katiba ya shirikisho la kisiasa itajumuisha wataalamu mbalimbali kutoka nchi zote tano wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
“Tumekubaliana juu ya taratibu na jinsi ya kuhakikisha kwamba ipo miongozo iliyowazi juu ya kuandaa rasimu hiyo ambayo hatimaye itafikia katika hatua ya mwisho ya kuundwa kwa shirikisho la kisiasa,” Waziri wa Serikali za Mitaa wa Rwanda, James Musoni alisema baada ya mkutano wa mawaziri mjini Kampala mwishoni mwa wiki.
Wakuu wa nchi za Rwanda, Kenya na Uganda Juni mwaka huu walikubaliana kuongeza kasi ya kufikia lengo la shirikisho la Afrika mashariki.
Pia katika mkutano uliofanyika Mombasa, Kenya, Agosti mwaka huu, Burundi nayo iliunga mkono hatua hiyo ambayo pia inalenga kuimairisha miundombinu chakavu ndani ya kanda hiyo ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo wa Kampala juu ya shirikisho la kisiasa ni wa kwanza wa aina yake ambapo maafisa waandamizi kutoka Rwanda, Kenya, Burundi na Uganda wamehudhuria tangu kikao cha utatu kilichofanyika mjini Entebe, Uganda Juni, mwaka huu.
Mawaziri kutoka nchi mbalimbali wananchama wa EAC waliopewa dhamana ya maandalizi ya shirikisho la kisiasa watatoa ripoti ya hatua iliyofikiwa mbele ya mkutano wa wakuu wa nchi za EAC utakaofanyika Oktoba, mjini Kigali, Rwanda.
Tanzania haimo katika mchakato wa shirikisho. Nchi hizo nne za EAC zinatumia baadhi ya vipembele katika mtangamano wa Afrika Mashariki ambavyo vinaeleza kwamba baadhi ya wananchama ndani ya jumuiya wanaweza kwenda kasi zaidi kuliko wengine katika baadhi ya masuala yanayohusu mtangamano.
Mahakama ya Afrika ya Mashariki (EACJ) ilitoa uamuzi mwaka 2009 kwamba hatua ya aina hii inaendana sawia na mahitaji ya muafaka katika kufikia maamuzi ndani ya EAC.