Na Joachim Mushi, Kirando, Nkasi
WAHAMIAJI haramu raia kutoka nchini Congo (DRC) wameanza kurejea nchini Tanzania ikiwa ni kipindi kifupi tangu Oparesheni Kimbunga ifanyike ambayo ilikuwa na lengo la kupambana na raia wanaoingia nchini Tanzania kinyemela na kufanya shughuli zao bila kufuata taratibu zinazotakiwa.
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na dev.kisakuzi.com katika Kata ya Kirando, Wilayani Nkasi Mkoa wa Rukwa umebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya raia kutoka nje ya nchi ambao wameingia nchini kinyume na taratibu za kawaida huku wakiendesha shughuli zao katika eneo hilo lililopo mpakani mwa Tanzania.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mtandao huu walisema tayari raia wengi wa Congo wamerejea nchini mara baada ya wao kupisha oparesheni kimbunga, ambayo iliwafanya wengi wao kukimbia na kurudi katika nchi zao.
“…Tayari wamerejea tena wahamiaji hawa haramu ambao wengi wanatoka nchi za Demokrasia ya Congo na Burundi, awali walikimbia wote mara baada ya kuanza kwa oparesheni kimbunga lakini sasa wamerejea na wanaendelea na kazi zao,” alisema mkazi mmoja wa Kirando kwa sharti la kutotajwa jina lake.
Alisema idadi kubwa wa raia hao huingia katika eneo hilo kwa kutumia njia ya maji, yaani Ziwa Tanganyika na kuja kufanya biashara na shughuli za kilimo; ambapo wengi wanadai wanavutiwa na hali ya utulivu wa taifa la Tanzania ukilinganisha na nchi zao.
Akizungumza na dev.kisakuzi.com Kaimu Mtendaji wa Kata ya Kirando, Revocatus Tinga alithibitisha baadhi ya wahamiaji hao haramu kuanza kurejea eneo hilo. “…Ni kweli Wakongo wameanza kurejea eneo letu kwa sababu wanasema wamezoea Tanzania, wanavutiwa na huduma za kijamii pamoja na amani iliyopo wanasema vitu kama hivyo kwao ni tatizo kubwa,” alisema Tinga.
Alisema wakati inaendeshwa oparesheni kimbunga idadi kubwa ya wahamiaji hao haramu walikimbia Kata ya Kirando na kutelekeza mashamba, nyumba na baadhi ya biashara zao, lakini wameanza kurejea baada ya kuhisi zoezi hilo limemalizika. dev.kisakuzi.com ilifanikiwa kutembelea Kijiji cha Mandakerenge eneo ambalo idadi kubwa ya wahamiaji wanaendesha shughuli za uvuvi na kuzungumza na baadhi yao ambao walijulikana kwa rafudhi zao kuwa ni raia wa Congo.