Wakili Mwale apelekwa Gereza la Kisongo

Moja la mabasi ambayo hutumika kuwabeba mahabusu kwenda gerezani.

Na Janeth Mushi, Arusha

HATIMAYE wakili maarufu mkoani hapa, Medium Mwale anayeshtakiwa kwa
kosa la uhujumu uchumi wa zaidi ya sh. bilioni 18 na kughushi nyaraka
aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Mkoa ya Mt. Meru kwa matibabu amepelekwa mahabusu katika Gereza Kuu la Mkoa la Kisongo.

Taarifa ambazo mtandao huu umezipata zinaeleza kuwa Jeshi la Polisi limefikia hatua hiyo baada ya kukamilisha taratibu za kisheria na kumkabidhi mshtakiwa huyo Magereza juzi majira ya saa 11 jioni, huku akiwa chini ya ulinzi mkali.

Taarifa zaidi zinadai baada ya taratibu hizo kukamilika Mwale alichukuliwa na kupelekwa Gereza Kuu la Mkoa wa Arusha lililopo eneo la Kisongo hadi hapo kesi yake itakapotajwa tena Agosti 31 mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha.

Juzi Wakili Mwale alisomewa mashtaka 13 akiwa wodini katika
Hospitali ya Mount Meru, yakiwemo ya uhujumu uchumi, kughushi nyaraka kwaajili ya kujipatia fedha kinyume cha sheria zaidi ya Sh bilioni 18 kkwakutumia kampuni sita tofauti.

Shtaka la kwanza hadi la tatu anadaiwa kughushi Januari 6 hadi
Januari 13, 2010 na kuhamisha fedha kutoka kampuni za Olive Green, Nyamao Mbeche Hollo, Gregg Motachwa, Ogembo Meetchel, John H. Adam na
Mosoto O. Hoye. Shtaka la tatu hadi 13 ni la uhujumu uchumi Februari 16, 2010 kwa kuhamisha zaidi ya Sh. bilioni 1.9 kutoka kampuni ya Ogambo Chacha na Gregg Motachwa Mwita.

Aidha hati hiyo ya mashtaka imedai shtaka la nne Machi 5, 2010 ni
kuhamisha Dola 200,000 za Kimarekani, shtaka la tano Machi 30,2010
kuhamisha dola 159,500 za Kimarekani wakati shtaka la sita anadaiwa
kulitenda Septemba 27, 2010 kwakuhamisha dola 5,500 za Kimarekani.

Inadaiwa kuwa shtaka la saba ni Novemba 2,2010 kuhamisha dola
1,246,624.84 za Kimarekani, shtala la nane Desemba 21, 2010 kuhamisha dola 416,000.02 wakati shtaka la tisa alilifanya Desemba 24, 2010 kuhamisha dola 521,000 za Kimarekani.

Shtala la kumi alilifanya Januari 17, 2011 alihamisha dola 808,000.02
za Kimarekani, shtaka la 11 Februari 9 mwaka huu alihamisha dola
527,000.02 za Kimarekani na shtaka la kumi na mbili, Julai 13, 2011 alihamisha sh. 330,000,000.

Baada ya Mwale kusomewa mashtaka hayo ambayo aliyakana yote huku
wakili anayemtetea, Loom Ojare akiiomba mahakama imrudishie baadhi ya
mali zake Mwale alizokuwa akizitumia ambazo zilikuwa zinashikiliwa na
polisi. Baada ya maombi hayo Hakimu, Charles Magesa alitoa amri kuwa baadhi ya mali hizo ambazo hazikuorodheshwa kwenye hati ya mashtaka zirudishwe kwa Mwale ambazo ni simu na gari la kifahari la mtuhumiwa aina ya BMW lenye namba za usajili T907 BTS.