Wakazi wa Wilaya ya Lindi Mjini Watakiwa Kujiunga na Huduma ya Mfuko wa Afya ya Jamii

MAMA JK AKISALIMIA MWANANCHI KWENYE MKUTANO WAKE CHIKONJE, LINDI

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa kijiji cha Kineng’ene kata ya Mtanda wilaya ya Lindi mjini kujiunga na huduma ya mfuko wa afya ya jamii (CHF) unaotolewa na Mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF) ili waweze kuepukana na gharama za matibabu za mara kwa mara wanazolipa pindi wanapougua wakati ambao hawana fedha.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa (NEC) toka wilaya hiyo aliyasema hayo jana alipokuwa akijibu swali la mkazi wa kijiji hicho Sophia Lihame kuhusiana na gharama za upatikanaji wa huduma ya afya wanazolipa kwenye mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika katika kijijini hicho.

Alisema kuwa gharama ya kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ambayo katika wilaya hiyo inajulikana kama tiba kwa kadi si kubwa ukilinganisha na huduma inayotolewa kwani familia ya watu sita inachangia shilingi 10000 katika halmashauri ya wilaya fedha ambayo inatumika kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mjumbe huyo wa NEC pia aliwataka wakazi wa kata hiyo kutoogopa kupima afya zao ili waweze kujua kama wamepata maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU) au la kwani kwa kufanya hivyo kutawawezesha kulinda kinga za miili yao.

Mama Kikwete alisema, “Kwa wale waliopata maambukizi ya VVU wasione aibu kujitangaza hadharani kwani ugonjwa huu hauuwi haraka kama maralia pia msiwanyanyapae watu wanaoishi na VVU kwani wenzenu wamepima na uzijua afya zao tofauti na nyinyi ambao hamjapima”.

Aidha Mama Kikwete pia aliwataka wananchi hao ambao ni wakulima wadogowadogo kufuata taratibu na kujiunga katika vikundi vya maendeleo ambavyo vitawawezesha kupata mkopo benki na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha na kuachana na dhana kuwa wakulima wadogowadogo hawakopesheki.

Kwa upande wake Meya wa wilaya hiyo Frank Magali alisema kuwa kutokana na tatizo la upugufu wa chakula katika wilaya hiyo Serikali imetoa tani 172 za chakula ambazo zitawasili baada ya mbili na kugawiwa bure kwa wazee na watu wasiojiweza ambapo wananchi wa kawaida watauziwa kwa bei naafuu.

Katika Mkutano huo wananchi walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaka kujua jinsi Serikali itakavyowasadia ili aweze kulipwa malipo ya pili ya korosho ya shilingi 600 kwa kilo, jinsi gani wakulima wadogo wadogowadogo wanaweza kupata mikopo, upatikanaji wa huduma za afya, upungufu wa chakula na upungufu wa walimu hasa wa shule ya msingi kwani shule ya msingi Kineng’ene ina walimu tisa wanaofundisha wanafunzi 640.

Mama Kikwete yuko katika ziara ya kichama ya siku saba katika wilaya ya Lindi mjini atatembelea kata zote 18 za wilaya hiyo kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mjumbe wa NEC.