Na Genofeva Matemu – MAELEZO
HOSPITALI ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Tekinolojia (IMTU hospital) kwa kushirikiana na Umoja wa Jamii ya watu kutoka India Bengali waliopo nchini Tanzania watatoa huduma ya upimaji afya bure jumapili Mei 26 mwaka huu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaoishi maeneo ya Mbezi Beach .
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa hospitali ya IMTU Dkt. Ali Mzige alipokua akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na afya ya mtoto na umuhimu wa maziwa ya mama hasa kwa watoto walio chini ya miezi 6 .
Dkt. Mzige amesema wanakusudia kupima uzito, presha na kutazama afya ya kinywa kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo watatumia vifaa maalumu vya upimaji presha kwa watoto hao.
“Tutapima uzito ambao takwimu zake ni Kg 10 kwa mtoto wa mwaka mmoja, Kg 11 kwa mtoto wa mwaka mmoja na nusu, Kg 12 mtoto wa miaka 2, Kg 13 kwa mtoto wa miaka miwili na nusu, Kg 14 kwa mtoto wa miaka 3, Kg 15 kwa mtoto wa miaka mitatu na nusu, Kg 16 mtoto wa miaka 4, Kg 17 mtoto wa miaka minne na nusu, na Kg 18 ni kwa mtoto wa miaka mitano”, amesema Dkt. Mzige.
Akirejea matokeo ya sensa ya mwaka 2012 Dkt. Mzige amesema matokeo hayo yalionesha kuwa asilimia 42 ya watoto chini ya miaka mitano hapa nchini wamedumaa, ambapo asilimia 16 wana uzito pungufu (Underweight) na asilimia 5 wamekonda (Marasmic) wako kwenye rangi nyekundu ya kadi za watoto za kliniki.
Aidha Dkt. Mzige ameishauri jamii kula lishe bora na kamili sababu lishe bora huanzia nyumbani hivyo ni jukumu la jamii kupata elimu ya chakula bora na mlo kamili wenye kujenga afya bora kwa watoto.
Zoezi la upimaji wa afya kwa watoto limeanza rasmi mwaka huu na linatarajiwa kufanyika kila mwaka au mara mbili kwa mwaka kwa kushirikiana na uhisani wa Bango Sangho jamii ya wahindi wanaoishi hapa nchini ambao wamekua wakitoa vifaa vya kupimia afya za watoto.