Na Joachim Mushi
WAKAZI wa Dar es Salaam jana waliendelea kuumia na mgomo wa wafanyabiashara wa mafuta ya petrol na dizeli, wanaoendesha mgomo kwa siku saba sasa wakipinga agizo la Serikali la kuwataka kushusha bei nishati hiyo tofauti na walivyokuwa wakiuza awali.
Jana hali ilikuwa ngumu zaidi kwa wasafiri, watoaji huduma za usafiri wa umma maarufu kama daladala na wamiliki wa magari ambao hutegemea nishati za mafuta hayo kuendeshea vyombo hivyo. Daladala nyingi zilishindwa kufanya kazi kama ilivyo kawaida baada ya baadhi ya madereva kukosa mafuta ya kuendeshea vyombo hivyo.
Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa dev.kisakuzi.com katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ulishuhudia vituo vingi vinavyouza mafuta ya petrol na dizeli vikiwa vimefungwa na madereva wa vyombo vya moto wakihaha kusaka mafuta hayo katika maeneo anuai ya jiji.
Wingi wa magari ulipungua barabarani tofauti na kawaida baada ya baadhi ya daladala na magari binafsi kushindwa kufanya kazi kwa kile kukosa nishati za mafuta zinazoendeshea vyombo hivyo. Foleni zilipungua kwa kiasi kikubwa tofauti na siku zote hata mida ambao baadhi ya barabara huwa na foleni kubwa.
Hata hivyo vituo vichache vya uuzaji mafuta ambavyo vilikuwa vikiendelea na kazi havikuwa msaada mkubwa kwa magari, kwani vinauza kwa mgawo, yaani mafuta ya sh. 10,000 kwa kila gari na vingi vilikuwa nje ya jiji la Dar es Salaam-kiasi ambacho hakikuwa msaada kwa daladala na vyombo vinavyotegemea mafuta mengi tofauti na kiasi kilichokuwa kikitolewa.
Thehabari.com ilishuhudia idadi kubwa ya wananchi wakiwa wamesimama katika vituo vya daladala hadi majira ya saa nne kasorobo usiku maeneo ya Posta Mpya, Mnazi Mmoja, Kariakoo, Ubungo na Mwenge wakisubiri vyombo vya usafiri bila mafanikio. Vyombo hivyo vingi havikuwa vikifanya kazi.
Bunge jana lililazimika kuacha Shughuli za kawaida za siku hiyo na kuanza kujadili nini cha kufanya juu ya mgomo huo kwa wafanyabiashara wa mafuta. Idadi kubwa ya wabunge waliochangia mjadala huo walionekana kuishangaa Serikali kwa kushindwa nguvu na wafanyabiashara hao, ambao wanaendelea kuwatesa Watanzania.
Wabunge wengi waliitaka Serikali kutumia nguvu zake na sheria kuwaadhibu wafanyabiashara wa mafuta kufuatia kukaidi maagizo ya Serikali na kufanya mgomo ambao unaendelea kuwatesa wananchi bila sababu za msingi.
Hata hivyo tayari Serikali imetoa saa 24 tangu jana jioni ikizitaka kampuni nne kubwa waingizaji wa mafuta nchini za BP, Engen, Oilcom na Camel Oil kujieleza kwanini zisiadhibiwe kwa kile kukiuka sheria ya mafuta nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja jana mjini Dodoma, alipokuwa akitoa taarifa bungeni. “Awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kulishukuru Bunge lako tukufu kwa kunipa fursa hii ya kutoa taarifa kuhusu hali ya biashara ya mafuta ya petroli hapa nchini.
Kama tunavyofahamu, mafuta ya petroli ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu kwani viwanda, vyombo vya usafiri, na huduma nyinginezo nyingi hutegemea mafuta na bidhaa zake. Bei ya mafuta inapopanda, bei zingine nyingi hupanda kwa mfano bei za usafiri zinapanda, bei za vyakula zinapanda, bei za bidhaa za viwandani zinapanda; nakadhalika”
Serikali inachukua hatua zifuatazo ili kuhakikisha kuwa mafuta ya kutosha yanapatikana sehemu zote nchini. Serikali kupitia EWURA inafuatilia mwenendo wa usambazaji wa mafuta kutoka katika maghala ya makampuni ya mafuta kwenda kwenye vituo vya mafuta; Serikali kupitia EWURA itachukua hatua za kisheria kwa kampuni zilizokiuka masharti ya leseni na kusababisha uhaba wa mafuta kwenye vituo vya kuuza mafuta nchini; “Leo (jana) Serikali kupitia EWURA imeipa leseni COPEC kampuni tanzu ya Serikali kupitia TPDC kuanza kufanya biashara ya mafuta mara moja; na Serikali kwa kupitia EWURA imekamilisha taratibu za uagizaji wa mafuta kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa mafuta yanapatika na kwa gharama nafuu zaidi wakati wote.
Waziri Ngeleja alisema kufuatia hali iliyojitokeza, EWURA imetoa Compliance Order kwa makampuni manne ambayo ni BP, Engen, Oilcom na Camel Oil, ambapo wanatakiwa watekeleze hatua zifuatazo: Mara moja wanatakiwa kuanza kutoa huduma katika maghala yao ikiwa ni pamoja na kuanza kuuza mafuta katika vituo vya rejareja ikiwemo vituo vilivyo chini ya miliki zao; Waache mara moja kitendo chochote kitakachosababisha upungufu wa makusudi wa mafuta ya petroli katika soko la Tanzania; na katika kipindi cha masaa 24 wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria dhidi yao kwa kukiuka matakwa ya Sheria ya Mafuta pamoja na Sheria ya EWURA.
“Mheshimiwa Spika, baada ya kuisha kwa muda uliotolewa na EWURA, adhabu stahiki zitatolewa kwa wahusika ikiwa ni pamoja na kusitisha ama kufuta leseni. …katika hali ya kawaida na kwa mujibu wa Sheria, mtu asiporidhika na maamuzi ya EWURA anapaswa kukata rufani katika Baraza la Ushindani (Fair Competition Tribunal). Hatua hii haijafuatwa hadi sasa na Serikali ingeshauri kwamba masuala kama haya ni vema yakafuata taratibu za kisheria,” alisema Ngeleja katika taarifa hiyo.