Na Mwandishi Wetu, Moshi
JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu wawili wakazi wa Kijiji cha Mamba kwa Makundi Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kukutwa na misokoto 91 ya bhangi.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Yusuph Ilembo, amethibitisha kukamatwa kwa watu hao Mei 21 mwaka huu majira ya saa sita usiku katika kijiji hicho wakifanya biashara hiyo haramu.
Akielezea mazingira ya tukio Kaimu Kamanda huyo alisema sungusungu wa Kijiji cha Mamba kwa Makundi wakiwa doria na viongozi wao walimkamata, Lukas Kiwelu (35) mkazi wa kijiji hicho akiwa na misokoto 10 ya Bhangi.
Kwa mujibu wa Kamanda Ilembo kijana huyo mara baada ya kukamatwa alisema wapo wengine wanaouza madawa hayo ya kulevya ambapo aliwapeleka sungusungu hao hadi kwa Hilary Ngowi (41) na alipopekuliwa alikutwa na misokoto 81 ya bhangi akiwa ameificha kwenye mfuko wa Rambo chini ya makreti ya Bia.
Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote poindi upelelezi utakapokamilika ili kujibu shtaka linalowakabili. Kufuatia tukio hilo kaimu kamanda amewataka wananchi mkoani Kilimanjaro kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo na kuhakikisha wanawafichua wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uuzaji wa madawa ya Kulevya ikiwemo bhangi kutokana na kwamba madawa hayo ni hatari sana kwa afya za binadamu.
Aidha aliwataka pia vijana kujiepusha na vitendo vya uuzaji na utumiaji wa madawa ya Kulevya kutokana na kwamba madawa hayo yanawaharibu kiafya na ni kosakisheria na la jinai kujihusisha na vitendio hivyo.