WAJUMBE wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) jana jijini Dar es Salaam walivutiwa na teknolojia mpya inayotumiwa kwa sasa na Shirika hilo katika utengenezaji wa kadi ya mwanachama wa NSSF. Teknolojia hiyo mpya (mobile POS) ya utengenezaji wa kadi ya mwanachama wa NSSF imerahisisha maradufu muda wa awali wa utengenezaji wa kadi ya mwanachama (smart card) kutoka takribani wiki moja hadi ndani ya saa moja kwa sasa.
Wakitembelea miradi mbalimbali ya NSSF jana jijini Dar es Salaam Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF walishuhudia teknolojia hiyo katika Tawi la NSSF Temeke, ambapo walishuhudia wateja wakihudumiwa na kupata kadi ya uanachama wa taasisi hiyo ndani ya saa moja tofauti na ilivyokuwa awali.
Akiwaelezea Wajumbe wa Bodi, Meneja Kiongozi wa NSSF Temeke, Yahaya Mhamali, ambapo teknolojia hiyo inatumika tangu mwishoni mwa mwaka jana, alisema imeboresha shughuli za huduma kwa wateja kwani kwa sasa mteja anapata kadi ya uwanachama ndani ya saa moja tofauti na awali ambapo ilichukua takribani wiki moja kabla ya mteja kupata kadi hiyo.
Alisema teknolojia ya ‘Mobile POS’ kwa sasa inawawezesha NSSF kwenda moja kwa moja na kifaa hicho ofisi walipo wateja wao na kuingiza taarifa za mtena, kuzihakiki na hata kutoa kadi ya mwanachama huyo kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali.
Alisema kwa wateja wanaokuja wenyewe ofisini na kuwa na taarifa zao hutengenezewa kadi ya uanachama ndani ya saa moja jambo ambalo limeongeza ufanisi kihuduma tofauti na ilivyo kuwa hapo awali. “…Sasa hivi mteja akija mwenyewe ofisini akiwa na taarifa zake sahihi anapata kadi yake ndani ya saa moja na kuondoka,” alisema Mhamali.
Wajumbe hao walishuhudia mmoja wa wateja aliyetambulika kwa jina la Ester Msalahi, ambaye ni mwalimu katika shule moja ya msingi ya binafsi akihudumiwa na kupatiwa kadi yake ya uanachama ndani ya saa moja, ambapo kadi hiyo ilikabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NSSF, Abubakar Rajabu huku akishughudiwa na wajumbe wa bodi na viongozi waandamizi ya shirika hilo katika ziara hiyo.
NSSF kwa sasa inatumia mfumo wa kompyuta wa kuwahudumia wateja katika ofisi hiyo ambapo mteja uchukuwa tiketi ya huduma katika mashine maalumu ambapo itampa maelekezo eneo analopaswa kuhudumiwa kwa wakati na kufuata utaratibu.
Aidha viongozi waandamizi wa NSSF walitembelea jengo jipya la NSSF linalojengwa eneo la Ilala ambalo litakuwa na ghorofa 20 kwenda juu huku likiwa na eneo la kuegesha magari la ghorofa nne ardhini. Ghorofa hilo linalojengwa kisasa ambalo litakuwa likitumiwa na NSSF Mkoa wa Ilala pia litakuwa na ofisi za kukodi, kumbi za mikutano benki na huduma zingine za kawaida za jamii mjini.
Akifafanua kwa wanahabari kuhusiana na ujenzi wa jengo hilo, Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi John Msemo alisema jingo hilo kwa sasa limefikia hatua za mwisho kukamilika kwani mafundi wanafanya matengenezo ya mwisho ili kumalizia ujenzi huo.
“…Jengo hili lipo katika hatua za mwisho kukamilika, sehemu kuwa ya ujenzi imemalizika na kinachofanyika sasa ni kuweka miundombinu kama ya maji, umeme na vutu vingine kama hivyo. Ghorofa hili pia kutakuwa na maeneo ya kupangisha wateja kwa shughuli mbalimbali…,” alisema Msemo.
Akifafanua zaidi Mhandisi Msemo alisema ujenzi wa ghorofa hilo la kisasa umegharimu shilingi za Kitanzania bilioni 40.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com