Wajumbe EAC wataka mipango ya rushwa iongezewe bajeti

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea

Na James Gashumba, Arusha- EANA

WAJUMBE wa Mkutano wa Kamati ya Sekta ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (ECA) wametoa changamoto kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kutenga fedha kwenye bajeti zao za kitaifa kila mwaka kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya rushwa.

Wajumbe hao walieleza kwenye maazimio yao mwishoni mwa kikao chao Arusha, Tanzania kwamba bajeti inayotolewa na EAC ni ndogo mno kuweza kukidhi haja ya watendaji waliomo kwenye vita dhidi ya rushwa.

Shirika la Huru la Habarai la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti kwamba katika maazimio hayo pia walizishauri nchi wanachama kutumia teknohama wakati wa kuwahoji washukiwa wa uhalifu wa rushwa kama mbinu moja ya kuimarisha taratibu za ulinzi wa ushahidi.

Mapema wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa EAC, anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Beatrice Kiraso alirejea wito wake kwamba kanda hiyo ya ECA, imedhamiria ‘’ kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya rushwa na kuzingatia maadili na utu katika suala zima la mtangamano wa katika kanda.’’

‘’Nahitaji kusisitiza kwamba jambo hili ndiyo nguzo kuu ya itifaki ya utawala bora na ni utekelezaji wa msingi muhimu wa Jumuiya.’’

Kiraso pia aliwajulisha wajumbe hatua iliyofikia mswada wa itafaki ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa kwa kuwadokeza kwamba tayari umepitishwa na Baraza la mawaziri na kukubaliwa na mkutano wa wakuu wa nchi kutiwa saini.

Kwa mujibu wa Kiraso mswada huo unatarajiwa kutiwa saini katika kikao maalum cha wakuu wa EAC kitakachofanyika hivi karibuni.

Kakao cha kamati ya Sekta ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa EAC kiliitishwa kwa lengo la kupata maendeleo ya hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa wa makubaliano yaliyofikiwa katika vikao vilivyotangulia vya Baraza la Mawaziri na kubadilishana uzoefu wa kitaifa, kikanda na dunia katika sekta hiyo.

Wajumbe wa kikao hicho wametoka katika idara na taasisi mbalimbali katika nchi tano wananchama wa EAC ikiwa ni pamoja na wakala wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, wizara za sheria na katiba na wizira zinazoshugulikia Jumuiya za Afrika Mashariki na utawala bora, wakaguzi wa serikali, ofisi za wanasheria wakuu wa serikali, mahakama za kupambana na rushwa, mashiraka ya kiraia na maafisa wa EAC.