Waislamu Watakiwa Kuepuka Kugawanywa na Kutengeneza Makundi Baina yao

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ALhaj Dk.Ali
Mohamed Shein,akisalimiana na Sheikh Alhad Mussa Salum,alipowasili
katika msikiti Masjid majmuatil Islamia,wa Temeke mwisho kuhudhuria
katika maulid ya Mtume Muhamad SAW.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
Wanamadrasatul Az-har ya Koma Kisiwani Dar es Salaam,wakisoma Qaswida
Ya swalatu Alan Nabii,katika Maulid ya Kumswalia Mtume Muhammad
SAW,yaliyofanyika jana katika Msikiti Masjid Majmuatil Islamia,wa
Temeke mwisho. .[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

WAUMINI wa dini ya Kiislamu wametakiwa kuwa na utamaduni wa kuzungumzia tofauti zinazotokea miongoni mwao na kuepuka kabisa kugawanywa na kuanzisha makundi yanayokwenda kinyume na maadili ya Kiislamu jambo ambalo halitoi taswira nzuri kwa dini hiyo.

Hayo yameelelezwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein katika hafla ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W), huko Masjid Majmuwatil Islamia, Temeke mjini Dar-es-Salaam.

Akitoa nasaha zake Alhaj Dk. Shein alisema kuwa waumuni wa dini ya Kiislamu wanapaswa kuendeleza mafundisho ya Bwana Mtume Mohammad (S.A.W) kwa vitendo ikiwa ni pamoja na kukaa na viongozi wao wa Kiislamu na kuzungumzia masuala mbali mbali yanayohusu changamoto zilizopo katika kuendeleza dini hiyo.

Alisema kuwa dini ya Kiislamu inasisitiza amani, masikilizano na usalama miongoni mwa waumini ikiwa ni pamoja na kuishi vyema na watu wasio Waislamu jambo ambalo Bwana Mtume Muhammad (S.A.W), alilifanya kwa mifano katika uhi wake alipokuwa akiishi Madina na hata Makka.

Aidha, aliwaomba Masheikh na Maimamu kuzisaidia Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapiduzi Zanzibar katika juhudi za kuendeleza amani na utulifu.

Alimpongeza sana Mufti wa Tanzania Sheikh Issa Shaaban Simba kwa juhudi zake katika kulitekeleza hilo pamoja na Sheikh wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Sheikh Alhad Mussa Salum ambae ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani ya Madhehebu ya Dini mbali mbali kwa juhudi zake.

Alhaj Dk. Shein alisema kuwa katika kutafakari namna bora zaidi ya kumkumbuka Mtume ipo haja katika kuendeleza mafundisho yake na mwenendo wake mwema huku dini ya Kiislamu ikisisitiza kuendele kushikilia miongozo miwili ambayo ni Qur-an na Sunna za Bwana Mtume.

Pamoja na hayo, Dk Shein alieleza wajibu wa kuwapa watoto na vijana elimu mbali mbali zenye manufaa kwani Uislamu umesisitiza sna umuhimu wa kutafuta elimu, jambo ambalo ni wajibu kwa Muislamu mwanamme na mwanamke.

Aidha, Alhaj Dk. Shein alikumbusha umma wa Waislamu waliohudhuria katika hafla hiyo kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwafunza watoto maadili mema na adabu kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya Kiislamu.

Katika hotuba yake hiyo Alhaj Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwataka Waumini hao kutekeleza wajibu wao katika kuwaepusha watoto na ushawishi wa ibilisi ambao siku zote huwa unawaongoza waja katika njia ya kumuasi Mwenyezi Mungu

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Shein alitoa shukurani kwa Mlezi wa Msikiti huo, Mheshimiwa Mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Imamu Mkuu Sheikh Alhad Mussa Salum na Bodi ya Wadhamini ya msikiti huo kwa kazi kubwa wanayoifanya katika mradi wa majengo ya mikiti yanayoendelea.

Nae Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mlezi wa msikiti huo, Alhaj Al Hassan Mwinyi akimkaribisha mgeni rasmi alisema kuwa nchi ya Tanzania ni kisiwa cha amani na utulivu hivyo kuna haja kuitunza ili na wengine waje kuirithi.

Alisema kuwa wananchi wote wana haki sawa na ni jambo la kushangaza wananchi hao wakaanza kubaguana kidini kwani kila mtu ana dini yake na kusisitiza haja ya kuishi pamoja na kupendana sanjari na kuvumiliana.

Alhaj Ali Hassan Mwinyi alikemea chokochoko za kidini na kuwataka waumini wa dini zote kuacha hasama na ugomvi miongoni mwao na kueleza kuwa kamwe hazitoipeleka nchi pahali.

Mapema akitoa salamu za wazee na wapenzi wa Mtume wa Mkoa wa Dar-es-Salaam Sheikh Majid Saleh aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kutoa ushirikiano wao katika kusimamia amani na utulivu iliopo nchini.

Aidha, alipongeza hal ya amani na utulivu iliypo anzibar hivi sasa na kusema kuwa mafanikio hayo yamepatikana kutokana na uongozi mahubuti wa Alhaj Dk. Shein.

Katika hafla hiyo pia, Alhaj Dk. Shein alikabidhiwa zawadi maalum na uongozi wa msikiti huo ambapo pia, na yeye alitoa shahada maalum kwa viongozi mbali mbali waliosaidia katika kusimania amani na utulivu iliyopo nchini.

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa dini, vyama vya siasa na serikali walihudhuria wakiwemo masheikh kutoka Misri, Pakistaan, Kenya pamoja na baadhi Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.