Mmoja wa waandamanaji akizungumza na vyombo vya habari kuelezea nia ya maandamano yao
Na Joachim Mushi
BAADHI ya waumini wa dini ya Kiislamu leo jijini Dar es Salaam wamefanya maandamano katika viwanja wa Kidongo Chekundu ikiwa ni hatua ya kuungana na Waislamu katika nchi mbalimbali kupinga filamu iliyotengenezwa nchini Marekani ikimkashfu kiongozi wao (Mtume) pamoja na dini ya Kiislamu.
Maandamano hayo yalianza majira ya mchana mara baada ya kumalizika kwa swala ya Ijumaa kwa misikiti mbalimbali hasa ile ya kati kati ya jiji, ambapo waumini waliongozana kuelekea katika Viwanja vya Kidongo Chekundi vilivyopo pembezoni mwa eneo la Mnazi Mmoja.
Taarifa za awali zilieleza awali waumini hao kupitia viongozi wao waliomba kibali cha kufanya maandamano kuelekea viwanja vya Jangwani lakini walizuiwa kutokana na uwanja huo kuwa na shughuli zingine. Baada ya kuzuiwa waliamua kuandamana kwenye eneo hilo bila kibali chochote lakini hakukuwa na kikwazo chochote.
Waandamanaji walionekana wameshika mabango yaliokuwa na ujumbe wa kuyalaani mataifa ya Marekani na Israel huku wakiitaka Serikali kufuta ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kutokana na filamu wanayoilalamikia kutengenezwa katika taifa hilo.
Taarifa za awali zilidai kundi hilo la waandamanaji lilipanga kuelekea zilipo balozi za Marekani jambo ambalo halikufanyika zaidi ya kuishia kuzunguka katika viwanja vya Kidongo Chekundu chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kilichokuwa tayari kudhibiti vurugu zozote.
Magasi ya FFU pamoja na asikari wa kawaida walikuwa wamesheheni eneo moja la viwanja vya Kidongo Chekundu wakiwa na vifaa vyote vya kudhibiti/kukabiliana na aina yoyote ya vurugu na walikuwa wamezuia waandamanaji hao kuvuka eneo hilo.
Baadha ya kuzunguka kwa muda huku wakiimba nyimbo za kulaani kitendo kilichofanyika baadhi ya viongozi wa vikundi hivyo vya maandamano walipanda na kutoa matamko ya kulaani kitendo kilichofanywa dhidi ya Mtume, na kwa pamoja walitoa tamko la kuitaka Serikali kutoa tamko dhidi ya kitendo kilichofanyika ndani ya wiki moja na kinyume cha hapo watafanya maandamano makubwa kulaani zaidi.