Na Mwandishi Wetu
WANAFUNZI waliohitimu darasa la saba mwaka 1988 Shule ya Msingi Muhimbili wametoa msaada wa viti vya kisasa 30, meza nane (9) na kufanya ukarabati ofisi ya walimu na ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo ambapo gharama za msaada huo kwa pamoja umefikia kiasi cha shilingi milioni 17.
Wakikabidhi msaada huo shuleni hapo leo jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa umoja huo wa wanafunzi wahitimu wa darasa la saba mwaka 1988, Bi. Usia Nkhoma Ledama alisema wanafunzi hao wapatao 80 waliamua kuchangishana fedha na kuamua kuisaidia shule yao ya zamani ikiwa ni kama shukrani kwa walimu na shule iliyowapa elimu ya msingi.
Alisema katika msaada huo kuna viti 29 na meza nane ambazo zimetengnezwa kisasa kwa ajili ya ofisi ya walimu ‘staff room’, kiti na meza ya kisasa ya ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo, pamoja na kufanya ukarabati wa ofisi ya walimu ikiwemo kupaka rangi, kukarabati dirisha na kufunga feni ili ifanane na thamani zilizowekwa.
Bi. Ledama alisema wanafunzi hao ambao wameanzisha umoja huo kupitia mtandao wa jamii (whatsapp)baada ya kukutana ndani ya miezi mitatu walikubaliana kufanya jambo moja la kuisaidia chochote shule yao ikiwa ni ishara ya shukrani ndipo walipofanya mawasiliano na kujua shule hiyo ilikuwa na uhaba wa viti pamoja na meza za walimu hivyo kuchangishana hadi kupata msaada huo.
“…Baada ya mjadala katika kundi letu la whatsapp kukubuka na kukumbushana maisha yetu ya shule ya msingi kukolea ndipo tukapata wazo kutoa msaada kwa shule yetu ya msingi kama alama ya shukrani yetu kwa malezi na elimu tuliopata hapa iliyoweza kutufikisha hapa leo, tarehe 7 mwezi Aprili mwaka huu (2015) sie tuliopo Dar es Salaam tukakutana kwa mara ya kwanza na kujadiliana namna ya kusaidia shule yetu,” alisema Bi. Ledama.
Kwa upande wake Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Balozi Kassim Mwawado aliwapongeza wanafunzi hao kwa kitendo cha kuguswa na kuamua kuikumbuka shule waliosoma na kuwaomba waendelee na moyo huo wa ushirikiano kwa masuala mbalimbali ili kujenga mshikamano zaidi baina yao.
Aidha aliushauri uongozi wa shule kuwa na eneo maalum la kuweka kumbukumbu kwa wanafunzi waliosoma shuleni hapo na kufanikiwa pamoja na matukio muhimu ambayo yatawajengea mwongozo mzuri wanafunzi na morali ya kufanya vizuri zaaidi katika masomo yao.
Naye Mkuu wa Shule ya Msingi Muhimbili wa sasa, Dafrossa Asenga akipokea msaada huo aliwashukuru wanafunzi waliojitolea na kuwataka wauendeleze umoja wao huo ili uweze kudumu na kushirikiana na kusaidiana kwa masuala mbalimbali ya msingi.
Hafla hiyo ya tukio la kukabidhi msaada huo pia iliwakutanisha baadhi ya walimu waliowafundisha wanafunzi hao mwaka 1988, baadhi ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka 1988, viongozi wa bodi ya shule, pamoja na wanafunzi na walimu wa sasa wa shule ya Msingi Muhimbili.