Na Joachim Mushi
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi leo jijini Dar es Salaam imetangaza msamaha kwa wahitimu 9,626 wa darasa la saba waliofutiwa matokeo kutokana na majibu yao kuwa na mfano usio wa kawaida na kuwataka kurudia mtihani huo mwaka huu.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Philipo Mulugo amesema Serikali imeamua kuchukua uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali. Naibu waziri huyo ametangaza kuwa msahama huo hauwahusu watahiniwa 107 waliofutiwa matokeo yao kutokana na kukutwa na majibu, kukariri darasa na makosa mengine kama hayo.
Mulugo amesema wizara yake itaunda tume ya kuchunguza udanganyifu katika mitihani na kutoa mapendekezo ya jinsi ya kudhibiti udanganyifu huo ambapo taarifa ya uchunguzi huo itatolewa mwishoni mwa mwezi aprili mwaka huu.
Kuhusu wahitimu wanaomaliza darasa la saba na kujiunga na shule za sekondari huku wakiwa hawajui kusoma na kuandika, Naibu Waziri huyo amesisitiza kuwa wanafunzi wote wa kidato cha kwanza watafanya jaribio ili kuwapima uwezo wao.
Amewaasa wazazi, walezi, walimu na jamii kwa ujumla kufahamu kuwa jukumu la utoaji, usimamizi na uendeshaji wa elimu ni la kila mdau na kuiasa jamii kwa ujumla kujiepusha na udanganyifu katika mitihani na kuwalea watoto katika misingi ya maadili mema, kujiamini na kujitegemea katika maisha yao.
Hata hivyo, Mulugo amesema Serikali inafanyia kazi suala la kiwango cha ada katika shule binafsi na kuwataka wananchi wawe na subira wakati serikali inashughulikia suala hilo.
Wizara ya Elimu na Mfunzo ya Ufundi, Desemba 14, 2011 ikitangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba, iliwafutia matokeo ya wanafunzi 9,736 kutokana na udanganyifu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, hatua ambayo ilizua malalamiko kutoka kwa wadau anuai.