Na James Gashumba, EANA
NAIBU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Beatrice Kiraso, amesema matatizo ya kiusalama yanayoikabili kanda hiyo hivi sasa yanahitaji nguvu za pamoja kuweza kuyakabili.
“Tukiwa pamoja tunakuwa na nguvu zaidi na hivyo kutuweka katika nafasi nzuri ya kuwashinda maadui zetu bila kupata vikwazo vyovyote,” Kiraso aliwaambia wajumbe wa mkutano wa kuandaa mswada kuhusu Utoaji Taarifa Mapema kuhusu Majanga katika EAC (EACWARN), mjini Entebbe, Uganda jana.
Ujumbe huo ulisomwa kwa niaba yake na Mtalaamu wa Masuala ya Amani na Usalama wa EAC, Leonard Onyonyi.
Alisema, hususan ni katika kanda yetu zaidi kuliko kwenye kanda nyingine, labda ni kutokana na ukaribu wa kijiografia, iko katika tishio la hatari mpya za kiusalama zaidi ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, uharamia, ugaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, madawa ya kulevya na silaha pamoja na uandaaji vijana katika makundi ya kiuhalifu kama vile Alshaababu.
Alizipongeza nchi wanachama wa EAC kwa kuunganisha nguvu zao kupambana na uhalifu kama huo kwa mujibu wa hutoba ya naibu Katibu Mkuu wa EAC, nakala yake iliyotumwa kwa Shirika Huru ya Habari ya Afrika Mashariki (EANA) leo.
“Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru kwa kujitoa kwa dhati kuimarisha sekta ya amani na usalama. Hii inatia moyo juhudi zetu za pamoja za kutaka kuwepo kwa amani, usalama na utulivu, mambo ambayo ni ya msingi kabisa katika kutaka kujiletea maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi katika jumuiya yetu ili kuwa na mtangamano uliofanikiwa katika EAC,” alisisitiza.
Alisema, maharamia katika siku za hivi karibuni wamekuwa ndiyo tishio kubwa la kiusalama kama walivyokuwa wakionekana kushirikiana kuvuruga usalama wa kanda hii na kusababisha kupanda kwa gharama za biashara na ufanyaji biashara. “Tunapenda kuzipongeza nchi wanachama kwa kuunganisha nguvu zao kupambana na maadui hao,” alisema.
Lengo kuu la kuandaa mswada huo wa EACWARN ni kusaidia mkakati wa upatikanaji wa taarifa za majanga mapema ili kuwezesha kufanyika kwa maandalizi ya kukabiliana nayo.