Wahimizwa Kujitokeza Kupima Ugonjwa wa Kisukari

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe.

Na Beatrice Lyimo – Maelezo

SERIKALI imetoa wito kwa kila mwananchi nchini kuhakikisha kwamba anapima afya yake mara kwa mara kwa kuwa ugonjwa wa kisukari unaweza usionyeshe dalili yoyote mapema ili kuweza kukabiliana na kupunguza athari za ugonjwa huo. Aidha Serikali imesisitiza kuwa endapo mtu atatambulika kuwa ana ugonjwa huo, atumie huduma za afya kulingana na ushauri wa atakaopewa na wataalam wa afya.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe leo alipokuwa anatoa tamko kuhusu Siku ya Kisukari Duniani itakayoadhimishwa Novemba 14, mwaka huu duniani kote yenye kauli mbiu “Ulaji unaofaa, huanza na mlo wa asubuhi”.

Siku ya kisukari duniani ilianzishwa baada ya kuona ugonjwa wa kisukari unaongezeka sana duniani kote na Tanzania kama nchi nyingine duniani huadhimisha siku hii kwa kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na ugonjwa huu, alisema Naimu Waziri.

“Ugonjwa wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu,” aliongeza Dk. Kebwe. Amebainisha kuwa asilimia 80 ya wagonjwa wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, na tafiti zinaonyseha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246 milioni duniani, mwaka 2012 wagonjwa milioni 371, mwaka 2013 wagonjwa milioni 382 ulimwenguni kote na mwaka 2013 kulikuwa na wagonjwa milioni 19.8 barani Afrika.
 
Aidha nchini Tanzania kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 ulionyesha kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari. Dk. Kebwe aliongeza kuwa takwimu za watoto wenye kisukari mwaka huu ni kati ya asilimia 15 mpaka 20 ya wagonjwa wa kisukari ambao wanatibiwa kwenye kliniki za hapa nchini.

“Lakini wapo wengine hawajitokezi kwenye kliniki kwa sababu mbalimbali zikiwemo imani potofu, gharama pamoja na umbali wa huduma za afya zilizopo,” aliongeza Naibu Waziri huyo.

Aidha Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) inayolenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani ya Nchi na wa kimataifa.

Tanzania inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011 la kuhakikisha magonjwa yasio ya kuambukiza yanapungua kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2025.