Wahariri watembelea Hifadhi ya Mikumi Morogoro

Baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wakiwa ndani ya Hifadhi ya Mikumi, wakiangalia vivutio mbalimbali vilivyomo ndani ya hifadhi hiyo.

WAHARIRI wa vyombo mbalimbali vya habari nchini, leo wamefanya ziara ya kutembelea Hifadhi ya Mikumi, ikiwa ni moja ya jitihada zinazofanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kuhamasisha utalii wa ndani na kujenga uhusiano mzuri na vyombo vya habari.

Wahariri hao wakiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kigazi, Katibu Mkuu wa Baraza la Habari nchini (MCT), Kajubi Mkajanga na baadhi ya maofisa waandamizi kutoka TANAPA, waliwasili Mbuga ya Mikumi majira ya asubuhi na kutembezwa katika mbuga hiyo kuangalia wanyama mbalimbali, ndege na viumbe wengine wanaopatikana eneo hilo.

Ziara ya wahariri hao ni mwendelezo wa warsha iliyoandaliwa tangu Alhamisi mjini Morogoro, ambapo mada mbalimbali juu ya masuala anuai ya hifadhi za taifa zilitolewa kwa wadau hao muhimu wa vyombo vya habari, ikiwa ni moja ya mpango kazi wa tanapa wa kejenga uhusiano mzuri na vyombo vya habari.

Leo timu hiyo ya wahariri inarejea mjini Dar es Salaam kuendelea na majukumu yao ya kawaida. Tayari TANAPA inaandaa utaratibu wa kuwashindanisha wanahabari pamoja na vyombo vya habari kupata mshindi anayeonekana kuripoti vizuri habari za shirika hilo ikiwa ni mkakati wa kutangaza vivutio vyetu na kuhamasisha utalii wa ndani.