WAHAMIAJI takribani 400, wengi wao wanaohisiwa kutoka nchini Somalia, wanahofiwa kuzama katika Bahari ya Mediterranean wakijaribu kuvuka kuelekea barani Ulaya. Kwa mujibu wa taarifa kutoka nchini Misri zinasema wahamiaji hao walikuwa wakitumia boti nne kusafiria.
Ndugu na jamaa wa baadhi ya wahamiaji hao wamesema baadhi ya wahamiaji hao waliokolewa na kikosi cha wana maji kutoka Ugiriki na sasa wapo nchini Ugiriki. Balozi wa Somalia nchini Misri amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na amesema bado wanatafuta taarifa zaidi za ajali hiyo.
Wakati huo huo; Korea Kusini imesema imepata taarifa kuwa Korea Kaskazini inajiandaa kufanya jaribio la tano la bomu la nyuklia, alisema Rais Park Geun-hye. Hata hivyo hakufafanua zaidi juu ya taarifa hiyo zaidi ya kuagiza jeshi la nchi yake kuwa tayari kwa tukio hilo.
Kumekuwa na ripoti katika vyombo vya habari nchini Korea Kusini kwamba kumeongezeka shughuli katika kituo cha majaribio ya silaha za nyuklia cha Korea Kaskazini cha Punggye-ri, ambapo majaribio ya awali yalitekelezwa. Iwapo Pyongyang itaendelea na kufanyia majaribio bomu la nyuklia, basi itakuwa ni kukaidi zaidi vikwazo vikali ilivyoongezewa na Umoja wa Mataifa mwezi jana.
“Tupo katika hali ya kutatanisha, hatujui iwapo Korea Kaskazini inaweza kufanya uchokozi kama njia ya kujitetea kutokana na kutengwa na jamii ya kimataifa na pia kuimarisha uungwaji mkono ndani ya nchi,” Bi Park aliambia maafisa wake wakuu wa jeshi, shirika la habari la Yonhap liliripoti.
Mwezi Januari, Korea Kaskazini ilifanya jaribio la nne la silaha za nyuklia na baadaye ikarusha kombora baharini. Hatua hiyo iliongeza hali ya wasiwasi katika rasi ya Korea. Waangalizi wanasema huenda jaribio hilo la bomu likafanywa kabla ya mkutano mkuu wa chama tawala cha Workers’ Party mjini Pyongyang mwezi Mei.
Wataalamu wanaamini Korea Kaskazini haina uwezo wa kiteknolojia wa kuweka silaha ya nyuklia kwenye kombora, ingawa imepiga hatua kubwa katika mpango wake wa nyuklia miaka ya karibuni.
-BBC