Wagonjwa Wapya 3,411 wa Saratani Wahudumiwa Ocean Road

NA MAGRETH KINABO- MAELEZO DODOMA
  8/5/2013
 
WAZIRI wa   Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa   jumla ya wagonjwa wapya wa saratani 3,411 wamehudumiwa na Taasisi ya Saratani Ocean Road.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma wakati Waziri huyo akiwasilisha hotuba yake  kuhusu  Makadrio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa mwaka 2013/2014  ya sh. 753,856,475,000 ambapo  aliomba Bunge lijadili kuidhinisha.

 Alisema wagonjwa hao walihudumiwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 ambapo wanaume ni 1,159 na wanawake ni 2,252. Hivyo wagonjwa 1,193 walitibiwa kama wagonjwa wa nje na wengine 2,218 walilazwa.

 Aliongeza kuwa hospitali hiyo ilihudumia wagonjwa 12,423 wa marudio katika kliniki, mbapo wanaume walikuwa ni 4,352 na wanawake ni 8,080.

 Aidha alifafanua kuwa jumla ya wanawake 8,765 walifanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na matiti.

Kati yao, 788 waligundulika na dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi na 23 walikutwa na saratani  ya matiti na walianza kupatiwa matibabu.