Na Immaculate Makilika- Dodoma
SERIKALI yawapongeza wafugaji wote nchini kwa mchango wao mkubwa unaoliwezesha Taifa kutoagiza nyama toka nje ya nchi na badala yake kuliingizia kipato kutokana na mauzo ya mifugo hai na nyama nchi za nje.
Hayo yamesemwa Bungeni leo na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi , Benedict Ole Nangaro ,wakati wa kipindi cha maswali na majibu, hata hivyo Naibu Waziri huyo alisema kwamba mwaka 2011/2012, ng’ombe 3,362 na mbuzi/kondoo 4,060 wenye thamani ya Sh. Bilioni 3.81 waliuzwa nje.
Aidha tani 31.6 za nyama ya ng’ombe ,tani 647 za nyama ya mbuzi na tani 151.8 za nyama ya kondoo ziliuzwa nje na kulingizia Taifa takribani Sh. bilioni 19.3
Fedha iliyookolewa kwa kutoagiza nyama kutoka nje haiwekwi kama akiba mahsusi bali hutumika kwa maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya mifugo.
Nchi yetu inajitosheleza kwa mahitaji ya nyama ambayo kwa mwaka tunazalisha wastani wa tani 462,686, kwa mchanganuo wa nyama ya ng’ombe tani 248,108, nyama ya mbuzi/kondoo tani 92,351, nyama ya nguruwe tani 39,676 na nyama ya kuku tani 82,551.
Hata hivyo, kutokana na mahitaji ya soko hususani wageni toka nje ,baadhi ya hoteli za kitalii na migodi huagiza tani 800 za nyama maalumu kwa mwaka ,kiasi kinachogharimu Sh. bilioni 10.2.
Serikali inaendelea kuwahimiza wafugaji kufuga kibiashara na kuzalisha nyama bora ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ikiwemo migodi.