MAHAKAMAya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imetathmini ushahidi wa upande wa mashtaka yanayowakabili watu 54, wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na kubaini kuwa wana kesi ya kujibu.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kufanya maandamano yaliyozuiliwa na polisi, kukusanyika isivyo halali, uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani. Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo ambaye alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashtaka na vielelezo, mahakama imeona kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu na kwamba wanapaswa kutoa utetezi wao.
Mapema wakili wa washtakiwa hao, Mohammed Tibanyendera aliiomba mahakama iwaachie huru washtakiwa kwa madai kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, umeshindwa kuthibitisha makosa dhidi ya washtakiwa.
Wakili Tibanyendera alidai kuwa, mashahidi wa upande wa mashtaka wote walikiri kuwa hakuna hata mmoja aliyewahi kuona tangazo la kuzuia maandamano. Pia alidai kuwa hakuna ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ukionyesha kuwa kulikuwa na maandamano na kwamba mashahidi wote waliithibitishia mahakama kuwa walishiriki katika kukamata washtakiwa kwa njia ya simu ya upepo ya polisi.
Wakili huyo pia alidai kuwa mikusanyiko haikuwa ya kuvunja amani na kwamba wala hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama kuwa alishuhudia uvunjifu wa amani ama malalamiko kutoka kwa majirani kuhusu hofu.
“Hii inadhihirisha kuwa mkusanyiko waliokuwa nao washtakiwa ulikuwa halali na hakukuwa na amri yoyote ile ya kuzuia watu kukusanyika katika Jamhuri ya Tanzania hapo Februari 15, mwaka huu,” alidai wakili huyo.
Pia wakili huyo wa kujitegemea alidai kuwa hakukuwahi kutolewa wakati wowote ule, amri ya kuzuia mkusanyiko na kwamba walizuia maandamano. Wakili Tibanyendera alidai kuwa ukamataji wa wateja wake, ulifanyika baada ya Swala ya Ijumaa, na kwamba watu walikamatwa katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Mkunguni na Makunganya.
Alifafanua kuwa waliokamatwa katika maeneo ya Mkunganya walikamatwa umbali wa mita 100 kutoka msikitini, DIT walikuwa karibu na kituo cha daladala na waliokamatwa katika eneo la Mkunguni walikuwa karibu na misikiti takriban mita tatu.
“Huu ni uwiano mkubwa wa kimazingira, tulitarajia tutapata ushahidi tofauti baina ya watu waliotenda kosa na waliokusanyika katika nyumba za ibada,” alidai wakili huyo wa utetezi.
Baada ya kumaliza kutoa hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Benard Kongola aliiomba mahakama iwaone washtakiwa kuwa wana kesi ya kujibu.
Hakimu Fimbo aliiahirisha kesi hiyo hadi leo washtakiwa watakapoanza kujitetea.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya upande wa mashtaka kupitia mawakili wa Serikali waandamizi, Benard Kongola, Nassor Katuga na Joseph Mahugo kufunga ushahidi wao. Upande wa mashtaka ulifunga ushahidi wake baada ya kupeleka mashahidi 10 mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya washtaka wakiambatanisha pia vielelezo 12.
Alidai kuwa Februari 11, mwaka huu alipokea barua kutoka katika Shura ya Maimamu, ikimwomba kibali cha kufanya maandamano ya kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). Alidai kuwa barua hiyo ilisainiwa na Sheikh Juma Idd na kwamba ndani yake pia ilikuwa inahoji sababu za kutokumpatia dhamana Sheikh Ponda.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz