Wafanyakazi SBL wawagagadua wahariri 1-0


Mgeni rasmi wa mchezo huo, Joseph Kulangwa ambaye pia ni Mhariri Mkuu wa Habari Leo (kulia) akisalimiana na mmoja wa wachezaji wa timu ya Serengeti Breweries, Teddy Mapunda kabla ya kuanza kwa pambano hilo, lililofanyika CCP Moshi.

Kilimanjaro,
WAFANYAKAZI wa Serengeti Breweries Ltd (SBL) mjini Moshi jana walikata ngebe za timu ya Jukwaa la Wahariri nchini baada ya kuwagagadua bao moja kwa bila. Mchezo huo wa kirafiki uliofanyika jana mjini Moshi baada ya Jukwaa la Wahariri kumaliza mkutano wao mkuu uliofanyika mjini Arusha, ulikuwa wa vuta ni kuvute muda.

Hata hivyo timu ya Serengeti ambayo muda wote ilicheza kwa kujihami ikiongozwa na mchezaji wao, Teddy Mapunda ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ilifanikiwa kupata bao hilo baada ya mshambuliaji wao hatari kuwazidi ujanja mabeki wa wapinzani wao.

Akizungumzia mchezo huo muda mfupi baada ya kumalizika kwa pambano, Kocha Mkuu wa Jukwaa la Wahariri, Masoud Sanani alisema wachezaji wake wameshindwa kucheza vizuri kutokana na hali ya hewa (baridi) kwani wao wamezoea kucheza kwenye hali ya hewa ya joto kali.

“Na jambo lingine tumecheza chini ya kiwango kutokana na kutofanya mazoezi muda mrefu…hili tumeliona na sasa tunatarajia kuanzisha programu ya mazoezi mfululizo ili kuwaweka sawa wachezaji wetu,” alisema Sanani.

Katika mchezo huo mchezaji wa Jukwaa la Wahariri, Sarehe Muhamed alikosa penati baada ya mshambuliaji wa kutegemewa wa timu hiyo, Kulwa Kauledia kukosa penati. Hadi mwisho wa mchezo SBL 1 na Jukwaa la Wahariri 0.