Wafanyakazi Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu Acacia Kahama Wachangia Damu

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Asa Mwaipopo akitoa damu. Kulia ni mtaalamu wa afya Rose Manyama

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Asa Mwaipopo akitoa damu. Kulia ni mtaalamu wa afya Rose Manyama.

 


Kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara,Sam Roesler na Mkuu wa Kitengo cha Utumishi Kampuni ya Acacia ofisi za London nchini Uingereza (kulia) wakichangia damu kwa ajili ya hospitali ya Mji wa Kahama.

WAFANYAKAZI wa Kampuni ya Uchimbaji ya dhahabu ya Acacia kupitia mgodi wa Buzwagi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wameanza zoezi la kuchangia damu kwa ajili ya kusaidia hospitali ya Mji wa Kahama inayokabiliwa na upungufu mkubwa wa damu hali inayochangia ongezeko la vifo hasa akina mama wakati wa kujifungua. Akizungumza na waandishi wa habari jana katika mgodi huo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Asa Mwaipopo alisema zoezi hilo litadumu kwa muda wa wiki moja kuanzia Julai 11 hadi Julai 16 Mwaka huu katika mgodi huo.

“Tarehe 14 mwezi Juni huwa ni siku ya kuchangia damu duniani, lakini sisi Buzwagi tumechagua wiki hii kuanzia tarehe 11, Julai hadi 16 Julai kuwa ndiyo kipindi chetu cha kuungana na wale wote walioshiriki katika uchangiaji wa damu siku ya damu duniani iliyokuwa na ujumbe wa “Toa Damu Changia Maisha”.

Alisema hospitali ya mji wa Kahama inakabiliwa na uhitaji mkubwa wa damu ambapo kwa mwezi zinahitajika takribani chupa 600 lakini damu inayopatikana pale ni takribani chupa 400 hali inayoonesha kuwa bado kuna hitaji kubwa la dam.u

“Sisi kama familia kubwa katika eneo la Kahama kwa maana ya Acacia Buzwagi kwa kutambua hilo, tumeandaa wiki hii iwe maalum kwa ajili ya wafanyakazi wetu kuchangia na kusaidia kupunguza upungufu wa damu katika hospitali ya Mji wa Kahama na tunaamini mchango wetu utasaidia kuokoa maisha ya watu wengi”,alisema Mwaipopo.

“Tunakusudia wiki hii kuchangia kiasa cha chupa 600,siku ya kwanza pekee tumepata chupa zaidi ya 100 …viongozi mbalimbali wa Acacia kutoka ofisi zetu za Dar es salaam, Johanesburg na London pamoja na mambo mengine waliyokuja kuyafanya nao watashiriki katika zoezi hili la uchangiaji damu “,aliongeza Mwaipopo.

Mwaipopo alisema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 50 ya uchangiaji wa damu duniani unafanyika katika nchi zilizoendelea, asilimia 50 ni kwa nchi zinazoendelea na kwamba idadi ya watu katika nchi zilizoendelea ni asilimia 20 na nchi zinazoendelea zenye idadi ya watu asilimia 80 uchangiaji wake ni asilimia 50.

Aliongeza kuwa uhitaji wa damu katika nchi zinazoendelea ni mkubwa mfano Tanzania takwimu zinaonesha kuwa kila wanawake l00,000 wanaojifungua, kati yao 400 wanapata changamoto zinazohitaji damu na hiyo haihusishi ajali au matukio mengine yenye uhitaji wa damu.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Kahama Dr. Joseph Ngowi mbali na kupongeza mgodi wa Acacia Buzwagi kwa namna ya kipekee walivyoweza kuchangia damu alismema wameonesha mfano wa kizalendo na wa kuigwa kwa makampuni na mashirika mbalimbali yanayotoa huduma katika jamii.

Alisema hospitali ya mji wa Kahama inahudumia wateja wengi wenye uhitaji mkubwa wa damu na kwamba damu ndiyo kiungo hasa kinachookoa maisha ya watu wengi.

“Takwimu tulizonazo hivi sasa ni kwamba uhitaji wa damu kwa siku katika hospitali yetu ni uniti 20 za damu na inafikia kipindi tunakuwa na uniti moja au mbili na wakati mwingine hakuna kabisa”,alieleza Dr. Ngowi.

Alisema zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi vinatokana na sababu ya kukosa damu au kupoteza damu inayohusiana na uzazi kwa hiyo katika zoezi hilo la ukusanyaji damu litasaidia kuokoa vifo vyao kwa zaidi ya asilimia 80 na matatizo mengine ikiwemo ajali na mahitaji mengine ya wagonjwa.

“Kwa mchango huu, kwa kujitolea huku kwa wafanyakazi wa kampuni ya Acacia ,itasaidia kuokoa maisha ya watanzania wengi wenye uhitaji wa damu,mikakati yetu ni kuendelea kukusanya damu na uchangiaji uwe endelevu katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika shule na tunatoa wito kwa mashirika,taasisi na watu mbalimbali kuendelea kuchangia damu”.

 


Katikati ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Asa Mwaipopo akizungumza katika ukumbi wa mikutano wa mgodi huo,kulia ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Kahama Dr. Joseph Ngowi. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Afya na Usalama Kazini katika mgodi wa Acacia Buzwagi,Dr. Antoinette George.

 


Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Kahama Dr. Joseph Ngowi akielezea changamoto ya damu katika hospitali hiyo ambapo alisema hivi sasa wana mkakati kabambe wa kukusanya damu katika maeneo mbalimbali.

 


Meneja Mkuu wa Mgodi wa Acacia Buzwagi Asa Mwaipopo akitoa damu.


Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Kampuni ya Acacia ofisi za London, nchini Uingereza Mark Morcombe akichangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya Watanzania.


Wataalamu wa afya wakisimamia zoezi la uchangiaji damu-Kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara,Sam Roesler na Mkuu wa Kitengo cha Utumishi Kampuni ya Acacia ofisi za London nchini Uingereza (kulia) wakichangia damu kwa ajili ya hospitali ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga.

Kushoto ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara,Sam Roesler na Mkuu wa Kitengo cha Utumishi Kampuni ya Acacia ofisi za London nchini Uingereza (kulia) wakichangia damu kwa ajili ya hospitali ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga.


Damu ikiwa imehifadhiwa katika mgodi wa Acacia Buzwagi. Picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog.