KUELEKEA kuwepo kwa kampeni mbalimbali zinazolenga kuboresha usafi wa mazingira na miundombinu kumeendelea kuwaamsha wadau na taasisi mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada hizo, ambapo kampuni ya mawasiliano ya Halotel imezindua kampeni ya wafanyakazi wake kufanya usafi katika maeneo yote yanayozunguka minara iliyojengwa na kampuni hiyo.
HALOGREEN, ndio jina la kampeni ambayo ina lengo la kuboresha mazingira yanayozunguka maeneo yaliyojengwa minara ya kampuni hiyo ya Simu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika eneo la ubungo maji, jijini Dar es Salaam, ambapo kuna moja ya minara ya Halotel, Meneja Uhusiano wa Kampuni hiyo, Stella Pius, amesema kampeni hiyo ina lengo la kuweka mazingira safi na salama kwenye maeneo yote ambayo imewekwa mitambo ya mawasiliano.
“Tunathamini umuhimu wa kutunza mazingira, Minara ya mawasiliano tuliyo ijenga ni ya teknolojia ya hali ya juu na ni rafiki kwa Mazingira, licha ya hivyo bado tunaona ni jukumu letu kuhakikisha tunaweka mazingira yanayozunguka minara yetu katika hali ya usafi,” Alisema na kuongeza.
Wafanyakazi wote kwa upande wetu tumeona kuna jambo ambalo tunaweza kulifanya hususan katika kulinda na kuyaweka mazingira yetu katika hali ya usafi hivyo tumeamua kujitolea kufanya usafi katika maeneo yote yanayozunguka minara yetu nchi nzima, Alisema Pius.
Pius, alihitimisha kwa kusema kuwepo kwa Mazingira rafiki na safi katika maeneo ya minara hiyo ambayo mingine iko katika maeneo ya makazi ya watu yatawezesha kuwa na jamii yenye afya na inayozingatia usafi wa mazingira.