Wafanyabiashara wa mirungi waja na mbinu mpya

Mirungi


Na Thomas Dominick, Musoma

WAFANYABIASHARA wa Mirungi wemegundua mbinu mpya ya kusafirisha madawa hayo ya kulevya pamoja na dawa mbalimbali za Binadamu zilizopitwa na wakati kutoka nchini Kenya kuja mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Wafanyabiashara hao bidhaa hizo haramu wametumia madumu ya mafuta ya kula ya lita tano, kumi na ishirini kwa kuyatoboa chini na kuyaziba kwa moto utadhani kuwa ni mafuta ya kula, Chupa za chai kwa kutoa yai la ndani, mabegi ya nguo na maboksi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kamishna Msaidizi Robert Boaz alisema kuwa wafanyabisahara hao walikamatwa katika kizuizi cha polisi eneo la Kirumi.

Kamanda Boaz alisema kuwa wafanyabishara hao walikamatwa kwa nyakati tofauti Aprili 30, mwaka huu katika mabasi ya kampuni ya Zakaria na Batco ambayo yanafanya safari zake toka Sirari kuelekea Mwanza.

Aliwataja wafanyabisahara waliokamatwa ni Faima Athmani (38), Esther Daniel (33) wote wakazi wa Nyambiti Jijini Mwanza wakiwa na kilo 93 za mirungi, Emanuel Alex (20) akiwa na kilo 30, na Ngofilo Ngereja (40) alikuwa na kilo 14.

“Wote hawa walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa raia wema ambao wamechoshwa na tabia mbaya za baadhi ya watu ambao wanakusudia la kuharibu amani nchini kwa kuuza madawa ya kulevya pamoja na kuuza dawa ya binaadamu yaliyopitwa na wakati,” alisema.

Kamanda Boaz alisema kuwa dawa mbalimbali za binaadamu zilikamatwa lakini hakuna mtu yeyote aliyejitokeza kuwa alikuwa anahusika nazo hivyo jeshi hilo kuzichukua na kuzifikisha kituoni kwa ajili ya hatua zaidi.

Dawa zilizokamatwa ni pamoja Alu, Amoxiline, Qunin Syrup, Sp, dawa za za usingizi, dawa za Kifua Kikuu ambazo tayari zimepitwa na wakati. Amewaomba wananchi wa mkoa huo kutoa ushirikiano na Jeshi hilo ili kuweza kufanikisha vita ya kuzuia uingizaji wa dawa za kulenvya pamoja na za binadamu zilizopitwa na wakati.

“Tunawaomba wananchi kutoa ushirikiano na Jeshi lao kwa kuwa watu wanaoathirika ni sisi wenyewe hivyo wakatae hali hii kwani polisi pekee hawawezi bila ushirikiano wao,” alisema Boaz.

Mirungi hiyo na dawa hizo zilikuwa zimetokea nchi ya jirani ya Kenya ambazo zilipita katika mpaka wa Sirari na kuingia nchini.
CHANZO: Binda News