Mwandishi Wetu, Mpanda
WAFANYABIASHARA wanaosafirisha mpunga na mahindi kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), kituo cha Mpanda wamegoma kulipa ushuru kwa Halmashauri ya Mji huo kwani wamekuwa wakitozwa mara mbili.
Akizungumza kuwawakilisha wenzake mjini hapa jana, Mussa Amijee mkazi wa Mkoa wa Tabora alisemawamekuwa wakinunua mazao yao maeneo anuai ya wilaya hiyo na Mkoa wa Rukwa na kutozwa ushuru na halmashauri husika.
Alisema wamekuwa akishangazwa kutozwa tena ushuru wanapofikisha mazao yao katika Halmashauri ya Mji wa Mpanda katika Kituo cha TRC kwa lengo la kuyasafirisha.
Alisema wamekuwa wakionesha stakabadhi ya malipo ya ushuru kutoka sehemu waliponunulia bidhaa zao lakini wahusika wamekuwa wakipinga, jambo ambalo linaleta utata na mgogoro kati yao na halmashauri ya mji huo.
Naye mfanyabiashara wa mahindi na mpunga Mpanda, Mussa Panduka alisema halmashauri ya mji imekuwa ikiwadai walipie ushuru wa sh. 800,000 kwa kila behewa la magunia 400, ambapo kila gunia wanatakiwa walipie sh. 1,000 kitu ambacho kinawaumiza kibiashara.
Kutokana na mgogoro huo baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wanasafirisha mabehewa 14 ya Mpunga kwenda mkoani Tabora mwishoni mwa wiki waligoma kulipa ushuru huo na kukamatwa na polisi, lakini waliendelea na msimamo wao wa kutolipa.
Naye Mkuu wa Shirika la Reli Kituo cha Mpanda, Nahoda Khatibu alisema wateja wake wamekuwa wakisumbuliwa wanapokuwa wanapakia mizigo yao huku wao wakiwa tayari wameshapokea fedha za kusafirishia mizigo yao.
Nahodha alisema hali hiyo inalisababishia shirika hilo hasara kwani wafanyabiashara wengi watakimbilia kusafirisha mizigo kwa njia ya barabara, ambapo wamekuwa hawadaiwi malipo yoyote tofauti na njia ya reli. Aliongeza kuwa ni vizuri halmashauri ya mji ikaandaa utaratibu wa kukusanya mapato nje ya maeneo ya kituo cha reli ili kuondoa usumbufu kwa wateja wa shirika hilo.
Akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mpanda, Joseph Mchina amesema wafanyabiashara hao wanahaki ya kulipa ushuru kulingana na sheria ndogo ya fedha ya Halmashauri ya Mji wa Mpanda Sheria Na. 9 ya mwaka 1982, ambayo inawataka wafanyabiashara wanaosafirisha mazao nje ya halmashauri kupitia njia ya reli kulipa ushuru wa huduma hiyo.