Wafanyabiashara Mwanza Kukumbwa Magonjwa ya Mlipuko

Wafanyabiashara wakipanga vichwa vya samaki vilivyokaushwa.

Wafanyabiashara wakipanga vichwa vya samaki vilivyokaushwa.

Na Kibada Kibada – Mwanza

WAFANYABIASHARA ya samaki na bidhaa nyingine za maliasili katika soko la Samaki la Mwalo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemeala Jijini Mwanza wako hatarini kupatwa na Magonjwa ya mlipuko hasa wakati huku mvua zinazoendelea kunyesha kutokana na changamoto ya uchafuzi wa mazingira uliopo katika soko hilo.

Mbali ya uchafuzi huo pia zipo changamoto nyingine za uhaba wa vitendea kazi na miundo mbinu mibovu ya kutolea maji kwenye meza za kupokelea samaki pamoja na mrundikano wa taka ngumu na taka nyepesi katika maeneo mbalimbali ya Soko hilo la Mwalo wa Samaki.

Upungufu wa vitendea kazi kwa wafanyakazi wanashughulikia usafi katika soko hilo hasa samaki ambapo wafanyakazi wanaparua samaki bila kuwa kinga yeyote kwenye mikono yao na wala mabuti ya kuvaa wakati wakiwa kazini hali inayowafanya wafanye kazi katika mazingira magumu. Changamoto hizo zimebainika hivi karibuni pale Madiwani wa Halmashauri ya Mpanda Mkoani Katavi walipofanya ziara ya mafunzo katika Mwalo huo wa samaki kwa lengo la kujifunza namna ya uendeshaji wa Mwalo.

Ziara hiyo iliwatembeza maeneo mbalimbali ya soko na kupata ufafanuzi wa kina namna ya uendeshaji wa Mwalo kutoka kwa Viongozi wa Soko hilo, Halmashauri na kutembezwa maeneo mbalimbali hadi kufika katika maeneo ya kupokelea na samaki na kujionea jinsi hali ya usafi wa soko ulivyo ambapo walikutana na changamoto hiyo ya uchafuzi wa mazingira kama uwepo wa taka ngumu na nyepesi.

Soko hilo la Mwaloni hali ya usafi hairidhishi kutokana na kurudikana kwa taka ngumu, taka nyepesi na miundo mbinu duni ya vitendea kazi kwa watenda kazi wanaoshughulika na shughuli za kila siku katika soko hilo ambalo limesheheni kila aina ya bidhaa hasa mazao ya majini kama samaki pamoja na mazao mengine ya kilimo kama matunda na mbogamboga.

Akizungumza na Madiwani waliotoka Halmashauri ya Mpanda kwenda kujifunza masuala ya mwalo Jijini Mwanza Afisa Uvuvi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Fabiani Maha ameleza kuwa ipo changamoto kubwa ya uzalishaji wa taka ngumu katika soko hilo kama inavyoonekana ingawa zinashughulikiwa kadiri inavyowezekana ingawa bado miundo mbinu bado ni changamoto.

Mbali ya changamoto ya miundo mbinu pia ameleza kuwa ameeleza kuwa soko linapokea na kuuza biashara za maliasili, kilimo na kuchukua takwimu za uvuvi, pia kutoa vibali vya uvui na ubora wa mazao ya uvuvi na ushuru wake. 
 
Awali Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza Mhandisi Lukaza Justini alieleza kuwa ziwa ni uchumi na maisha na soko hilo lilijengwa mwaka 2006 kwa gharama ya shilingi bilioni sita na shirika la misaada la kijapani JAICA.

Mhandisi Lukaza akaeleza kuwa soko linalohudumia wakazi wa Mwanza, Mikoa ya jirani na wale wa ndani na nje ya nchi ambazo ni Kenya, Uganda, Kongo DRC, Rwanda na Burundi pamoja na Sudani Kusini kwa sasa dagaa wa Mwanza na samaki wameonekana kupata soko katika nchi za Asia.