Wafanyabiashara Mpanda wasota wakisubiri treni

Injini ya trani

Mpanda,

BAADHI ya wafanyabiashara wa mazao walioweka kambi katika kituo cha Reli cha mjini Mpanda, wakisubiri kusafirisha mazao yao wameingiwa na hofu ya uwezekano wa kuharibika kwa mazao yao na kupata hasara ya mamilioni ya fedha.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi jana mjini hapa, wafanyabiashara hao walisema iwapo uongozi wa Shirika la Reli hautachukua hatua za haraka kuwezesha kusafirishwa kwa mazao yao takriban tani zaidi ya 4500 za mahindi na mpunga kuna hatari ya kunyeshewa na mvua zinazotarajiwa kuanza siku za karibuni hivyo kuharibika.

“Tumelalamika sana sasa sijui hawa viongozi hawasikii kilio chetu au Serikali inataka tupate hasara, kwani hali ikiendelea hivi kuna hatari ya mazao yetu kunyeshewa na mvua ambayo kwa kawaida huwa inaanza mapema mwezi ujao eneo la Mpanda…matokeo yake ni kupata hasara na mitaji yetu ya biashara kuporomoka,” alisema, Yombo Emmanuel mmoja wa wafanyabiashara hao.

Licha ya hofu ya mvua wafanyabiashara hao ambayo wanatoka mikoa ya Tabora, Mwanza na Shinyanga, pia wamesema kutokana na kukaa kwa muda mrefu tangu Mei mwaka huu katika kituo hicho wakisubiri kusafirisha mazao, hali ya maisha kwa upande wao inazidi kuwa mbaya kutokana na kuingia gharama ambazo hawakuzitegemea za kuendelea kuishi mjini Mpanda.

Akizungumza hali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Mpanda, Dk. Rajabu Rutengwe alisema amefanya mawasiliano na uongozi wa juu wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, ambao umedai tatizo lililopo ni kukosekana kwa injini za kutosha, lakini hatua za makusudi zinafanywa kupata injini ili kumaliza tatizo la msongamano mkubwa mazao hayo.

Aidha, hivi karibuni baadhi ya wafanyabiashara hao wapatao 50 walilazimika kulala kwenye mataruma ya reli kuizuia treni ya mizingo isiondoke kwenye kituo cha Shirika la Reli Mpanda wakiushinikiza uongozi wa shirika hilo kusafirisha mazao yao katika gari moshi hilo badala ya Tumbaku.

Chanzo: Jambo Leo